Kenya yasimama na Morocco mgogoro wa Sahara Magharibi
(last modified Tue, 27 May 2025 06:33:10 GMT )
May 27, 2025 06:33 UTC
  • Kenya yasimama na Morocco mgogoro wa Sahara Magharibi

Kenya imesema inaunga mkono mpango wa Morocco wa kulipa eneo linalozozaniwa la Sahara Magharibi uhuru wa kujitawala chini ya mamlaka ya utawala wa kifalme wa nchi hiyo ya Afrika Kaskazini, ikiungana na idadi inayoongezeka ya nchi za Kiafrika, Kiarabu na Magharibi ambazo zimeelekeza uungaji mkono wao kwa Rabat katika mzozo huo wa miongo mitano.

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mazungumzo kati ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi hizo mbili mjini Rabat, Kenya imesema inauona mpango wa Morocco kuwa suluhisho pekee la kuaminika na la kweli na njia pekee endelevu.

Morocco inapendekeza mfumo wa mamlaka ya dani kujitawala  kwa eneo la Sahara Magharibi chini ya serikali kuu ya Rabat, huku Harakati ya Polisario ikisisitiza kufanyika kwa kura ya maoni kuhusu kuamua hatima ya eneo hilo.

Kenya, baada ya miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi mbili na Morocco, pia ilifungua ubalozi huko Rabat jana Jumatatu.

Morocco, nchi inayoongoza kwa uzalishaji wa fosfeti na mbolea, imekubali kuharakisha mara moja usafirishaji wa virutubisho vya udongo nchini Kenya, huku nchi hizo mbili zikipanga kushirikiana katika nishati mbadala, utalii, uvuvi, usalama na masuala ya kitamaduni na kidini, imesema taarifa hiyo ya pamoja.
Waziri wa mambo ya nje wa Morocco, Nasser Bourita amewaambia waandishi wa habari kuwa msimamo wa Kenya kuhusu Sahara Magharibi, ambao aliuita "kadhia ya kitaifa", umesaidia kuongeza msukumo mpya katika mahusiano baina ya nchi hizo mbili.

Mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu tangu mwaka 1975, unaikutanisha Morocco, ambayo inachukulia eneo hilo kama lake, dhidi ya mrengo wa Polisario unaoungwa mkono na Algeria, ambao unatafuta taifa huru katika eneo la jangwa.

Morocco ililitwaa eneo kubwa la Sahara Magharibi, koloni la zamani la Uhispania mwaka 1975 na tangu wakati huo imekuwa katika mzozo na mapigano na Harakati ya Polisario, inayoungwa mkono na Algeria, ambayo inapigania kuasisi nchi huru katika eneo hilo na kukomesha uwepo wa serikali ya Rabat.