Raia wa mashariki mwa Kongo watakiwa kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amewatolea wito raia wa mashariki mwa nchi hiyo kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi ujao.
Rais Joseph Kabila amewataka raia wa mashariki mwa Kongo khususan wakazi wa mkoa wa Kivu ya Kaskazini wajiandikishe kwa wingi katika zoezi lilioanzishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo ili wapatiwe kadi za kupigia kura kwa ajili ya uchaguzi ujao. Maeneo mengi na vijiji vinavyopatikana katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini katika miaka ya hivi karibuni yameshuhudia mashambulizi ya waasi wa Uganda. Rais wa Kongo Alhamisi iliyopita alifanya mazungumzo na Rais Yoweri Museveni wa Uganda kuhusu suala la ukosefu wa amani mashariki mwa Kongo lililosababishwa na waasi wa Uganda.
Marais hao wawili pia walikubaliana kubadilishana taarifa kuhusu harakati za waasi wa Uganda. Uchaguzi wa Rais nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unatazamiwa kufanyika mwezii Novemba mwaka huu.