Aug 07, 2016 13:13 UTC
  • Makabiliano kati ya jeshi na wabeba silaha Nigeria yaua 19

Watu 19 wameuawa katika makabiliano makali kati ya askari wa jeshi la serikali na kundi la wabeba silaha katika jimbo la Niger nchini Nigeria.

Habari zinasema kuwa, askari 11 wa Nigeria wameuawa katika makabiliano hayo yaliyofanyika katika eneo la Bosso jimbo la Niger. Kanali Sani Usman, msemaji wa jeshi la Nigeria amesema operesheni hiyo imejiri baada ya vyombo vya kijasusi nchini humo kupata taarifa kuwa kuna kundi la wabeba silaha na wezi wa mifugo linalowahangaisha wakaazi wa miji ya Kopa, Dagma na Gagaw katika jimbo hilo.

Askari wa Nigeria wakishika doria

Amesema kuwa, wavamizi 9 wameuawa katika makabiliano hayo na wengine wapatao 57 wametiwa nguvuni na kwamba uchunguzi dhidi yao unaendelea. Kanali Sani Usman ameongeza kuwa wanajeshi wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika wamenasa silaha kadhaa za wavamizi hao zikiwemo bunduki 13 za AK-47, bastola 9, bunduki 45 za kujitengenezea, mapanga 122, mikuki, mishale na nyuta.

Ramani ya Nigeria

Kwa mujibu wa jeshi la Nigeria, kundi hilo la wabeba bunduki na silaha nyingine hatari ndilo limekuwa likihusika na visa vya utekaji nyara katika siku za hivi karibuni katika mji wa Abuja.

Mbali na hujuma za waasi, wezi wa mifugo na makundi ya wabeba silaha, Nigeria imekuwa ikikabiliwa na wimbi la mashambulizi ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram.

Tags