Upinzani Zambia: Uchaguzi mkuu hautakuwa huru na wa haki
Kinara wa upinzani nchini Zambia ameituhumu serikali ya nchi hiyo kuwa inatumia sheria kandamizi ili kuwawekea mbinyo wapinzani na kuzuia kampeni zao, na kusisitiza kuwa uchaguzi mkuu wa Alkhamisi ijayo hautakuwa huru na wa haki.
Kiongozi wa chama cha upinzani chenye ushawishi mkubwa nchini humo Hakainde Hichilema amesema wafuasi wa chama tawala cha Patriotic Front (PF) wanachochea ghasia na kuwatishia wafuasi wa upinzani ili wasifanye kampeni za kipindi cha lala salama.
Hata hivyo, licha ya tuhuma hizo za upinzani, rais wa zamani wa Nigeria Goodluck Jonathan, anayeongoza timu ya waangalizi wa Umoja wa Afrika amesema joto la kisiasa na taharuki zimepungua kwa kiasi kikubwa baada ya serikali kupitia Tume ya Uchaguzi kusitisha kampeni kwa muda wa siku 10. Aidha amewataka wanaogombea viti mbalimbali wawe tayari kukubali matokeo.
Itakumbukwa kuwa, serikali ya Zambia ilitangaza kusitisha kampeni za uchaguzi mkuu katika baadhi ya maeneo ya nchi kutokana na kushadidi mgogoro na machafuko ya kisiasa mjini Lusaka. Kampeni hizo zilisimamishwa kati ya Julai 9 na 18 mjini Lusaka na katika eneo la Namwala, kusini mwa mji mkuu huo.
Rais Edgar Lungu anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kinara wa chama cha upinzani cha UPND, Hakainde Hichilema, baada ya kukabana koo katika uchaguzi wa mwaka jana. Rais Lungu alishinda kiti hicho Januari 2015, baada ya kuitishwa uchaguzi uliofanyika mapema baada ya kifo cha Michael Sata, Oktoba 2014.