Wananchi wa Morocco waandamana kulaani jinai za Israel
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i128544-wananchi_wa_morocco_waandamana_kulaani_jinai_za_israel
Maelfu ya wananchi wa Morocco waliingia mitaani jana Jumamosi kushiriki maandamano ya kutangaza mshikamano wao na wananchi wa Palestina katika Ukanda wa Gaza, sanjari na kulaani kampeni ya mauaji ya kimbari ya Israel, ambayo ipo katika mwezi wake wa 21 sasa.
(last modified 2025-10-20T07:03:11+00:00 )
Jul 20, 2025 12:22 UTC
  • Wananchi wa Morocco waandamana kulaani jinai za Israel

Maelfu ya wananchi wa Morocco waliingia mitaani jana Jumamosi kushiriki maandamano ya kutangaza mshikamano wao na wananchi wa Palestina katika Ukanda wa Gaza, sanjari na kulaani kampeni ya mauaji ya kimbari ya Israel, ambayo ipo katika mwezi wake wa 21 sasa.

Maandamano hayo yaliyoandaliwa na asasi ya kiraia ya 'Morocco Initiative for Support and Aid to Palestine' yalipitia katika barabara kadhaa kuu za mji wa Tangier na kuhitimishwa katikati mwa jiji.

Waandamanaji walilaani vikali mipango ya Israel ya kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina katikaUkanda wa Gaza, na kuendelea kwa mashambulio ya utawala huo wa Kizayuni dhidi ya wakazi wa Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

Washiriki wa maandamano hayo wakiwa wamebeba picha za Msikiti wa al-Aqswa na bendera za Palestina, walipiga nara za kulaani jinai za jeshi la Kizayuni katika Ukanda wa Gaza na kutaka kutumwa misaada ya kibinadamu katika ukanda huo.

Kadhalika waandamanaji hao sambamba na kulaani jinai na mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza, wametoa mwito wa kukomeshwa mara moja uhusiano wa nchi yao na Israel.

Maandamano hayo yameshika kasi katika miaka michache iliyopita hususan tangu kuanza Vita vya Gaza na jinai kubwa zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi.

Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, wananchi wa Morocco mbali na kulaani jinai za Israel dhidi ya Wapalestina, mara kadhaa wametoa mwito wa kufutwa makubaliano ya kuwa na uhusiano na utawala wa Kizayuni