Maandamano ya kutaka kulindwa wanahabari wa Gaza yafanyika Afrika Kusini
Waandishi wa habari wa Afrika Kusini na wafanyakazi wa vyombo vya habari wameongoza maandamano huko Sea Point jijini Cape Town, wakishinikiza kupewa ulinzi zaidi waandishi wa habari wa Palestina huko Gaza, sanjari na kutangaza mshikamano na wenzao waliouawa katika ukanda huo wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Maandamano hayo ya jana Jumapili ambayo waandaaji walisema yalivutia washiriki zaidi ya 2,000, yamejiri kufuatia shambulio la anga la Agosti 10 kwenye hema nje ya Hospitali ya Al-Shifa ya Gaza, lililoua shahidi waandishi watano wa televisheni ya Al-Jazeera, na mwanahabari mmoja wa kujitegemea.
Maandamano hayo yaliandaliwa na jumuiya ya Wanahabari Dhidi ya Ubaguzi wa Rangi (JAA) na Kampeni ya Mshikamano na Palestina, kwa msaada kutoka kwa vikundi vingine vikiwemo Mothers4Gaza, Wayahudi wa Afrika Kusini kwa Palestina Huru, na Wafanyakazi wa Afya kwa Palestina.
Waandishi wa habari wa Afrika Kusini wamelaani kile walichokitaja kuwa hatua ya Israel ya kuwalenga wanahabari wa Kipalestina kwa kufichua uhalifu wa kivita na mauaji ya kimbari. JAA inashutumu "mauaji ya vyombo vya habari" huko Gaza, ikizishutumu vyombo vya Magharibi kwa kukuza simulizi za Israel huku wakinyamazisha sauti za Wapalestina.
"Tumeghadhabishwa na vyombo vya habari vya Magharibi ambavyo vimerudia uwongo wa Israel bila kuchunguza huku vikiwa vimenyamazisha sauti za Wapalestina, jambo ambalo limeruhusu mauaji haya ya kimbari kuendelea," amesema mwanachama wa JAA, Deshnee Subramany.
Kundi hilo pia limekosoa vyombo vya habari vya Afrika Kusini kwa kushiriki katika safari za propaganda zilizofadhiliwa kwenda Israel bila kufichua vyanzo vya ufadhili wa ripoti zao.
Waandamanaji hao wametaka kuachiliwa kwa waandishi wa habari wa Kipalestina waliozuiliwa huko Gaza na Ukingo wa Magharibi, kukomesha marufuku ya vyombo vya habari iliyowekwa na Israel, na kuruhusiwa waandishi wa habari wa kigeni kuingia Gaza.