Luteni Jenerali Buratai: Boko Haram wanakaribia kushindwa kikamilifu
Kamanda Mkuu wa jeshi la Nigeria Tukur Yusuf Buratai amesema kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram linakaribia kushindwa kikamilifu.
Buratai ametangaza leo kuwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram linakaribia kushindwa kikamilifu na kwamba wanamgambo wa kundi hilo hawana uwezo tena wa kufanya vitendo vya kigaidi kama ilivyokuwa huko nyuma.
Luteni Jenerali Buratai ameashiria operesheni ya kijeshi la jeshi la Nigeria katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo na kueleza kwamba hatua ya jeshi na vikosi vya ulinzi imesaidia kupunguza mashambulio ya Boko Haram na kwamba hata nguvu za kujihami na kupambana za kundi hilo la kigaidi zimepungua sana.
Toleo la Jumamosi iliyopita la gazeti la Vanguard linalochapishwa katika mji wa Lagos lilichapisha ripoti na kueleza kuwa zaidi ya watu 30,000 wameuawa hadi sasa nchini humo kutokana na mashambulio ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram, mbali na mamia ya nyumba na maeneo ya vijiji yaliyochomwa moto na kundi hilo.
Katika miaka ya karibuni, mashambulio ya kundi la Boko Haram ambalo ngome yake kuu iko katika eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria yamezilenga pia nchi jirani za Chad, Cameroon na Niger.../