Shirika la Uhamiaji la Somalia na jitihada za kupambana na misimamo mikali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i130546-shirika_la_uhamiaji_la_somalia_na_jitihada_za_kupambana_na_misimamo_mikali
Shirika la Uhamiaji la Somalia linafanya kazi kwa bidii kupambana na vitendo vya uchupaji mipaka na misimamo mikali na kuimarisha usalama katika mipaka ya nchi hiyo kwa kushirikiana na washirika wa kimataifa.
(last modified 2025-09-08T07:32:12+00:00 )
Sep 08, 2025 07:32 UTC
  • Mustafa Sheikh Ali Dhuhulow
    Mustafa Sheikh Ali Dhuhulow

Shirika la Uhamiaji la Somalia linafanya kazi kwa bidii kupambana na vitendo vya uchupaji mipaka na misimamo mikali na kuimarisha usalama katika mipaka ya nchi hiyo kwa kushirikiana na washirika wa kimataifa.

Haya yamebainishwa na Mustafa Sheikh Ali Dhuhulow Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Uhamiaji la Somalia (ICA) ambalo ni moja ya taasisi kubwa za nchi hiyo ya mashariki mwa Afrika inayofanya kazi kote nchini ikiwa na wafanyakazi zaidi ya 1,400. Ofisi kuu ya shirika hilo ipo Mogadishu, mji mkuu wa Somalia. 

Shirika la Uhamiaji la Somalia ambalo liliasisiwa mwaka 1946 lilifanya kazi chini ya Kitengo cha Polisi ya Somalia cha Upepelezi wa Jinai (CID) na baadaye likawa chini ya Shirika la Taifa la Ujasusi na Usalama (NISA) na kisha likawa sehemu muhimu ya vyombo vya usalama vya ndani ya nchi. 

Dhuhulow amesema Shirika la Uhamiaji la Somalia  "linafanya kazi kwa bidii sana" kupambana na watu wenye misimamo mikali, huku wafanyakazi waliofunzwa vyema wakishirikiana kwa karibu na vyombo vya usalama vya ndani na washirika wa kimataifa.

" Kwa hakika tunajaribu kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wetu ili kuhakikisha kwamba Shirika la Uhamiaji la Somalia  linaweza kufanya kazi na dunia nzima. Tunahakikisha kuwa hakuna wasafiri haramu wanaosafiri kutoka Somalia au kuingia Somalia," amesema Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo.