Kushadidi hatua za wapinzani wa kisiasa Kongo dhidi ya serikali
Hatua za kupinga serikali za wapinzani wa kisiasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimepamba moto tangu kurejea nchini mwanasiasa mkongwe ambaye pia ni kiongozi wa upinzani nchini humo mzee Etienne Tshisekedi.
Etienne Tshisekedi kiongozi wa wapinzani wa serikali ya Kongo hivi karibuni alimfukuza kazi Bruno Mavungu mjumbe wa chama cha upinzani cha Muungano kwa ajili ya Demokrasia na Maendeleo ya Jamii kwa tuhuma za kumuunga mkono Rais Joseph Kabila. Tshisekedi mwenye umri wa miaka 83 hafai kugombea tena katika uchaguzi ujao wa rais baada ya kushindwa na Joseph Kabila katika uchaguzi wa rais mwaka 2011. Hii ni katika hali ambayo Joseph Kabila amejipanga kugombea tena kiti cha rais katika uchaguzi wa Novemba mwaka huu kinyume na kipengee cha katiba ya Kongo.
Sababu hiyo ilimfanya Rais Kabila mwezi Novemba mwaka jana apendekeze kufanyika mazungumzo ya kitaifa ili kuandaa uwanja wa kufanyika uchaguzi wa rais mwaka huu. Katika hali ambayo harakati za kisiasa za wapinzani nchini Kongo DR zimeshika kasi, hatima ya mazungumzo ya kitaifa ya nchi hiyo imesalia kuwa kitendawili huku baadhi ya weledi wa mambo wakisema kuwa si jambo lililo mbali kutokea vita vya ndani nchini humo. Umoja wa Mataifa pia umevitolea mwito vyama vya upinzani na serikali ya Kinshasa kufikia mapatano ya kitaifa. Kwa mujibu wa pendekezo hilo, wawakilishi wa serikali na wa vyama vya upinzani wanapasa kukaa pamoja na kujadili namna uchaguzi huo wa rais uliozua msuguano utakavyofanyika.
Duru ya pili ya kuwepo madarakani Rais Kabila inamalizika tarehe 20 mwezi Disemba mwaka huu huku anga ya kisiasa huko Kongo ikizidi kuwa mbaya siku baada ya siku kutokana na kukaribia muhula huo; na ndio maana Rais Joseph Kabila ametaka kuhuishwa vyama vya kisiasa nchini humo. Aidha Rais Kabila amewashajiiisha wakazi wa eneo la Butembo katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi ujao akiwa ziarani mkoani humo hivi karibuni. Pamoja na hayo yote baadhi ya weledi wa mambo wanaamini kuwa Rais Kabila hana uwezo wa kuvihuisha vyama vya kisiasa huko Kongo.
Kabila ambaye alipendekeza mpango wa kufanyika mazungumzo ya kitaifa baina ya vyama vya kisiasa vya nchi hiyo lengo likiwa ni kudhamini mazingira mazuri ya kufanyika uchaguzi mkuu kwa amani na utulivu, amekabiliwa na masharti kutoka wapinzani. Wapinzani wanataka kuachiwa huru wafungwa wote wa kisiasa huko Kongo. Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa Joseph Kabila alinufaika sana na mgawanyiko na hitilafu zilizokuwepo kati ya vyama na makundi ya kisiasa ya upinzani katika chaguzi za mwaka 2006 na 2011.
Mzee Etienne Tshisekedi ambaye haruhusiwi kugombea katika uchaguzi ujao wa rais nchini Kongo, mwaka huu anaonekana kufanya juhudi kubwa za kuleta umoja na mshikamamo kati ya vyama vya upinzani ili kumuarifisha mgombea mmoja wa upinzani atakayechuana na Kabila. Shakhsia maarufu kama Vitaly Kamerhe, Kengo wa Dondo na Nzanga Mobutu mwana wa kiume wa dikteta wa zamani wa Kongo yaani Zaire ya zamani ni miongoni mwa wagombea wanaotazamiwa kuteuliwa na mrengo wa upinzani kuchuana na Joseph Kabila.