Guterres atoa wito kwa Eritrea na Ethiopia kuheshimu makubaliano ya mpaka
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ijumaa, amezitaka Eritrea na Ethiopia kurejea kwenye dhamira ya makubaliano yaliyomaliza rasmi uhasama kati ya mataifa hayo mawili ya Pembe ya Afrika miaka 25 iliyopita, akionya kuwa mvutano unaoibuka upya unaweza kuhatarisha amani ya eneo.
Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wa Katibu Mkuu, Stephane Dujarric, ilielezwa: “Leo ni kumbukizi ya miaka 25 ya Mkataba wa Algiers, mkataba muhimu wa amani uliomaliza rasmi mgogoro wa mpaka kati ya Eritrea na Ethiopia na kuweka msingi muhimu wa mahusiano ya amani kati ya mataifa hayo mawili.”
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa mkataba huo uliweka “mifumo ya kuweka mipaka ya pamoja,” na pia “ulithibitisha tena misingi ya mamlaka kamili ya kitaifa na ardhi kwa mataifa yote mawili,” kwa uungwaji mkono wa jumuiya ya kimataifa.
Dujarric aliongeza kuwa: “Miaka saba iliyopita, viongozi wa nchi zote mbili walihuisha tena dhamira yao ya amani kupitia tamko la pamoja, ishara ya nguvu ya mazungumzo na ushirikiano.”
Katika kipindi hiki cha mvutano unaorejea, Guterres amezitaka “Eritrea na Ethiopia kurejea kwenye maono ya amani ya kudumu na kuheshimu mamlaka na mipaka ya kitaifa kama yalivyoainishwa katika Mkataba wa Algiers, na kuimarisha jitihada za kujenga uhusiano mwema wa ujirani.”
Kiongozi huyo wa UN pia amehimiza pande zote mbili “kuendelea kushirikiana na wadau wa kikanda na kimataifa kuendeleza ushirikiano wa maendeleo kwa manufaa ya wote.”
Eritrea na Ethiopia zilitia saini Mkataba wa Algiers baada ya vita vikali kati ya majirani hao wawili mwaka 1998–2000, vilivyosababisha vifo vya watu kati ya 70,000 na 80,000 kutoka pande zote.
Baadaye, tume ya kimataifa ya mipaka iliamua kuwa eneo la Badme—lililokuwa kitovu cha mgogoro—ni mali ya Eritrea, huku pia ikiamuru Eritrea kuilipa Ethiopia fidia kwa shehena kubwa za bidhaa za Ethiopia zilizokamatwa katika Bandari ya Assab.