UN kuchunguza radiamali ya walinda amani kufuatia kushambuliwa hoteli moja S/Kusini
Ban Ki-moon Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameanzisha uchunguzi kuhusu tuhuma zinazowakabili askari jeshi wa kulinda amani huko Sudan Kusini (UNMISS) kwamba walishindwa kuchukua hatua za haraka kukabiliana na shambulio la watu wenye silaha dhidi ya hoteli moja huko Juba.
Watu waliokuwa wamevalia sare wakiwa na silaha waliishambulia hoteli ya Terrain tarehe 11 mwezi Julai huko Juba mji mkuu wa Sudan Kusini na kuua mwandishi habari mmoja na kubaka raia kadhaa. Ban Ki-moon ameshtushwa na matokeo ya awali ya kamati ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa iliyopewa kazi ya kuchunguza shambulio lililofanywa na watu wenye silaha katika hoteli hiyo, wakati yalipoibuka mapigano kati ya vikosi vitiifu kwa Rais Salva Kiir na wapinagaji wanaomuunga mkono Makamu wake wa zamani Riek Machar. Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa Ban Ki-moon amesikitishwa na tuhuma kwamba wanajeshi wa kulinda amani wa umoja huo waliopo Sudan Kusini hawakuchukua hatua ipasavyo kuzuia shambulio hilo na kesi nyingine za udhalilishaji wa kijinsia zilizofanywa huko Juba. Kwa msingi huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa tayari ameanzisha uchunguzi maalumu huru kuhusu suala hilo.