Polisi yatumia mabomu kuzima maandamano Zimbabwe
Maafisa wa polisi nchini Zimbabwe wametumia mabomu ya kutoa machozi na maji yenye kuwasha kuzima maandamano ya makumi ya watu wanaopinga azma ya Benki Kuu nchini humo ya kufufua matumizi ya noti za nchi hiyo.
Waandamanaji hao walinuia kufanya maandamano katika barabara za mji mkuu Harare na kumalizia katika jengo la Benki Kuu, lakini wametawanywa na maafisa wa polisi waliotumia mabomu ya kutoa machozi na kuwanyunyizia maji ya kuwasha.
Waandamanaji hao wamesikika wakipiga nara kuwakosoa Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo, Waziri wa Fedha Patrick Chinamasa na Gavana wa Benki Kuu nchini humo John Mangudya wanaoshinikiza kufufuliwa matumizi ya noti hizo, ambazo waandamanaji hao wanasema ni sawa na karatasi za shashi.
Benki Kuu ya Zimbabwe ilisema kufikia mwezi Oktoba mwaka huu, itafufua matumizi ya sarafu ya nchi hiyo, kutokana na uhaba wa dola, hatua ambayo Rais Mugabe alipongeza na kudai kuwa itazuia wahalifu wanaopania kwenda nchini humo 'kuvuna dola.'
Haya yanajiri siku moja baada ya viongozi wa mrengo wa upinzani wakiongozwa na Morgan Tsvangirai, kiongozi wa chama cha MDC na Bi Joyce Mujuru, makamu wa zamani wa rais, kufanya mkutano mkubwa mjini Harare na kutoa wito wa kuungana vyama vyote vya upinzani ili kuiongoza Zimbabwe.
Katika siku za hivi karibuni Zimbabwe imeshuhudia wimbi la maandamano ya wapinzani kufuatia kuongezeka mgogoro wa kiuchumi, kijamii na pia ukatili wa polisi dhidi ya raia.