Kujisalimisha maelfu ya wanachama wa Boko Haram kwa jeshi la Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i13510-kujisalimisha_maelfu_ya_wanachama_wa_boko_haram_kwa_jeshi_la_nigeria
Kanali Rabe Abubakar, Mkurugenzi wa taarifa za ulinzi za jeshi la Nigeria amesema, hivi karibuni wanachama wapatao 8,000 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko wamejisalimisha kwa hiyari yao kwa jeshi la nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 18, 2016 12:45 UTC
  • Kujisalimisha maelfu ya wanachama wa Boko Haram kwa jeshi la Nigeria

Kanali Rabe Abubakar, Mkurugenzi wa taarifa za ulinzi za jeshi la Nigeria amesema, hivi karibuni wanachama wapatao 8,000 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko wamejisalimisha kwa hiyari yao kwa jeshi la nchi hiyo.

Askari wa jeshi la Nigeria wamefanikiwa kuwatimua na kuwarejesha nyuma wanamgambo wa kundi hilo katika jimbo la Borno lililoko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Kanali Rabe Abubakar

Katika miaka ya karibuni Nigeria imekabiliwa na vitisho vingi vya usalama. Wanamgambo wa kundi la Boko Haram upande wa kaskazini mashariki, wanamgambo wanaopigania kujitenga upande wa kusini mashariki, harakati ya kupigania eneo la Niger Delta mamlaka ya kujiendeshea mambo yake katika upande wa kusini mwa nchi na mivutano ya kikabila katika majimbo ya katikati ni miongoni mwa changamoto kubwa za kiusalama zinazoikabili serikali ya Abuja. 

Rais Muhammadu Buhari

Baada ya Rais Muhammadu Buhari kushika madaraka ya nchi mwezi Aprili mwaka uliopita wa 2015 alitoa ahadi kwa wananchi kuwa ataling'oa na kulitokomeza kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram katika majimbo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Hivi karibuni Wizara ya Ulinzi ya Nigeria ilisisitiza kuwa hatua zozote za kutaka kuvuruga amani katika maeneo tofauti ya nchi hiyo zitagonga ukuta. Inavyoonesha, mbali na Boko Haram, vitisho hivyo vinayakusudia pia makundi ya harakati ya kupigania ukombozi wa eneo la Niger Delta na lile la Walipizaji Kisasi wa Niger Delta ambayo yameanzisha harakati za kupigania eneo hilo kuwa na mamlaka ya kujiendeshea mambo yake na kupatiwa fungu kubwa zaidi la pato la mafuta yanayochimbwa kwa wingi katika eneo hilo.

Wanamgambo wa Niger Delta

Operesheni za jeshi la Nigeria zinalilenga zaidi kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram, ambalo katika miaka ya karibuni limevuruga amani katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa nchi na kupanua wigo wa mashambulio yake hadi ndani ya ardhi za mataifa jirani na Nigeria. Kundi hilo ambalo kuanzia katikati ya mwaka 2014 liliweza kudhibiti sehemu ya jimbo la Borno; hadi mwezi Januari mwaka uliopita liliweza kunyakua pia udhibiti wa maeneo mengi zaidi kutoka mikononi mwa jeshi la Nigeria. Pamoja na hayo, upinzani mkali wa jeshi uliwazuia wanamgambo wa kundi hilo la kigaidi na kitakfiri kuutwaa mji wa Maiduguri, makao makuu ya jimbo la Borno na kitovu cha kundi hilo. Kwa mtazamo wa wadadisi wa mambo ushirikiano na uratibu wa pamoja wa muungano wa majeshi ya nchi za eneo ni sababu muhimu ya mafanikio ya kijeshi iliyopata Nigeria.

Uzinduzi wa kikosi cha pamoja cha kupambana na Boko Haram

Mwaka uliopita, nchi za Niger, Chad, Cameroon na mwenyeji Nigeria ziliunda kikosi cha pamoja cha askari 8,700 kwa madhumuni ya kulitokomeza kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram ambalo limekuwa tishio kwa uthabiti wa eneo hilo na Afrika kwa jumla. Operesheni za mashambulio ya jeshi la Niger katika maeneo ya Diffa na Bosso kandokando mwa mpaka wa pamoja wa nchi hiyo na Nigeria yamekuwa na taathira pia kwa mafanikio kiliyopata kikosi cha pamoja cha majeshi ya mataifa kadhaa kinachopambana na Boko Haram.

Mashambulio ya Boko yamevuka mipaka ya Nigeria

Baadhi ya wajuzi wa mambo wanasema, siasa za Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria katiika mbinu za kupambana na Boko Haram zimekuwa na taathira kubwa zaidi. Buhari, ambaye ni Jenerali wa zamani wa jeshi anatumia tajiriba na uzoefu wa kijeshi wa Jenerali Yakubu Gowon, ambaye aliongoza operesheni za jeshi  wakati wa vita vya ndani katika kipindi cha kati ya mwaka 1960 hadi 1970.

Wanamgambo wa Boko Haram

Kujisalimisha kwa hiyari yao wanachama wapatao 8,000 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram ni bishara njema ya kutimuliwa na kutokomezwa kundi hilo la kigaidi ambalo mbali na kuteketeza roho za maelfu ya watu limesababisha pia hasara kubwa ya mali na ya kiuchumi kwa serikali ya Nigeria pamoja na majirani zake.../