Unicef: Watoto wanajiunga na makundi ya waasi Sudan Kusini
Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umesema unatiwa wasiwasi na kujiunga watoto na makundi yenye silaha huko Sudan Kusini.
Unicef imesema kuwa tangu kuanza mwaka huu wa 2016 zaidi ya watoto 650 wa Sudan Kusini wamejiunga na makundi ya wabeba silha. Unicef imeongeza kuwa watoto elfu 16 huko Sudan Kusini wamejiunga na makundi yenye silaha tangu kuanza mgogoro wa ndani nchini humo mwaka 2013.
Vita vya ndani vilianza huko Sudan Kusini mwezi Disemba mwaka 2013 baada ya Rais Salva Kiir wa nchi hiyo kumtuhumu aliyekuwa makamu wake, Riek Machar kuwa alifanya jaribio la kumpindua. Hata hivyo Machar kiongozi wa waasi mwezi Aprili mwaka huu alirejea katika mji mkuu wa nchi hiyo Juba ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya amani ya nchi hiyo na akachaguliwa kuwa Makamu wa Rais Salva Kiir baada ya kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa.
Mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba umeathiriwa na wimbi jipya la mapigano ya umwagaji damu kati ya vikosi vya askari watiifu kwa Rais Salva Kiir na wale wanaomuunga mkono aliyekuwa makamu wake, Riek Machar tangu tarehe 7 mwezi Julai mwaka huu.