UN: Machar yupo salama nchini Kongo DR
-
Farhan Haq
Riek Machar kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini na makamu wa zamani wa Rais wa nchi hiyo amekimbilia katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Hayo yameelezwa na Umoja wa Mataifa.
Msemaji wa umoja huo Farhan Haq amesema kuwa viongozi wa Kongo wamekiagiza kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini humo (MONUSCO) kisaidie kumhamisha Machar na familia yake kutoka sehemu moja karibu na mpaka wa Sudan Kusini na kumpeleka katika eneo salama. Haq amesema kuwa kikosi cha MONUSCO hakikuhusika katika kumondoka Riek Machar huko Sudan Kusini.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, Machar amekabidhiwa kwa maafisa husika wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kwamba kuhamishwa kwake huko kumefanyika kwa sababu za kibinadamu na kwa ridhaa yake. Amesema makamu huyo wa zamani wa Rais wa Sudan Kusini alikuwa hatarini na kwamba amepatiwa msaada wa kitiba aliohitajia.
Wakati huo huo James Gatdet Dak ambaye ni msemaji wa Riek Machar amesema kuwa wapiganaji wanaomuunga mkono mwanasiasa huyo wamefanikiwa kuzima kile alichokitaja kuwa ni jaribio la Rais Salva Kiir la kutaka kumuuwa Machar.
Riek Machar aliondoka katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba na kuelekea kusikojulikana baada ya kushadidi mapigano kati ya wafuasi wake na jeshi la serikali linalomuunga mkono Rais Salva Kiir.