Unicef yatadharisha kuhusu kujiunga watoto na makundi ya kigaidi
Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (Unicef) umetangaza kuwa watoto zaidi ya elfu 16 wamejiunga na makundi ya wabeba silaha huko Sudan Kusini na katika mwaka huu pia watoto zaidi ya 650 wamejiunga na makundi ya wanamgambo nchini humo.
Justin Forsyth Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Unicef ametahadharisha kuhusu suala hilo na kusisitiza kuwa tangu kuanza mwaka huu wa 2016 hadi sasa zaidi ya watoto 650 huko Sudan Kusini wameajiriwa na makundi yenye silaha, huku watoto wengi pia wakisalia kuwa wakimbizi kutokana na vita na mapigano ya miaka kadhaa nchini humo.
Miaka kadhaa imepita sasa tangu Sudan Kusini ikabiliwe na vita vya ndani na hadi kufikia sasa raia wengi wa nchi hiyo wameuawa, kujeruhiwa au kutumiwa vibaya kwa anwani mbalimbali. Weledi wa mambo wanasema kuwa watoto wamekuwa wahanga wakubwa na kudhurika zaidi katika miaka kadhaa ya hivi karibuni; huku wengi wa watoto hao wakitekwa nyara na makundi ya wanamgambo wenye silaha na kutumiwa katika mizozo ya kivita au kutumiwa vibaya kijinsia.
Si huko Sudan Kusini pekee, bali mapigano yanayojiri katika nchi nyingi duniani yamepelekea watoto kudhurika pakubwa.
Takwimu zinaonyesha kuwa watoto wengi Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wametekwa nyara na makundi yenye silaha na kutumiwa kwenye oparesheni mbalimbali za kijeshi.
Kuongezeka makundi ya wanamgambo na harakakati za kigaidi barani Afrika pia kumesababisha aghalabu ya watoto kutumiwa katika hujuma za kigaidi na mashambulizi ya kujiripua.
Huko Nigeria kundi la Boko Haram limeiba idadi kubwa ya watoto katika vijiji mbalimbali vya nchi hiyo na kisha kuwatumia katika oparesheni za kujiripua kwa mabomu. Aidha huko Somalia kundi la wanamgambo wa al Shabab linawatumia watoto katika oparesheni zao za kigaidi.
Umoja wa Mataifa uliwahi kutahadharisha kuwa kushtadi machafuko katika pembe mbalimbali duniani kufuatia kuongeza vita ulimwenguni, kunawatia katika hatari kubwa watoto ambao baadaye hutumiwa kama askari jeshi.Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa si tu kuwa suala la kuwatumia watoto katika oparesheni za kijeshi ni tishio kuu kwa kundi hilo, bali watoto wengi katika nchi hizo wanashuhudia jinai chungu nzima zisizoelelezeka na hivyo kuathirika pakubwa kisaikolojia.
Hata kama Umoja wa Mataifa na taasisi nyingine za kimataifa zinazohusika na kudhamini haki za watoto zimetaka kuchukuliwa hatua za haraka na za kimataifa ili kukomesha utumiaji watoto katika oparesheni za kijeshi na wakati huo huo kuyatolea mwito makundi yanayozozana katika maeneo yaliyoathiriwa na machafuko na mizozo ya kivita kuchukua hatua katika fremu ya sheria za kimataifa, lakini hali hiyo inaonekana kuendelea kuwakumba watoto katika nchi nyingi. Weledi wa mambo wanasisitiza kwamba juhudi za kimataifa zinapaswa kufanyika ili kurejesha amani duniani na kuhitimisha mizozo ya ndani au ya kimataifa. Ni katika mazingira kama hayo tu ndipo watoto wataweza kupata fursa ya kuwa na maisha bora na kuishi katika hali ya utulivu wa kiroho na kisaikolojia.