Afrika Kusini yalaani vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i137754-afrika_kusini_yalaani_vita_vya_marekani_na_israel_dhidi_ya_iran
Ronald Lamola, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, amefanya mazungumzo ya simu na Seyyed Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambapo amesisitiza msimamo wa nchi yake wa kulaani vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
(last modified 2026-04-03T07:06:48+00:00 )
Apr 03, 2026 03:39 UTC
  • Ronald Lamola, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, na Seyyed Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Iran
    Ronald Lamola, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, na Seyyed Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Iran

Ronald Lamola, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, amefanya mazungumzo ya simu na Seyyed Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambapo amesisitiza msimamo wa nchi yake wa kulaani vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

Katika mazungumzo hayo awali Lamola amewasilisha salamu za rambirambi  kufuatia kuuawa shahidi kwa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, pamoja na  maafisa, makamanda wa ngazi za juu na raia wa Iran katika mkondo wa uvamizi wa kijeshi wa Marekani na Israel. Pia amebainisha kuwa serikali na watu wa Afrika Kusini wanashikamana na serikali na wananchi wa Iran wakati huu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa shukrani kwa ujumbe wa rambirambi na pole pamoja na msimamo wa Afrika Kusini wa kulaani mashambulizi ya Marekani na utawala wa kibaguzi wa Israel dhidi ya Iran. Aidha, amesisitiza umuhimu wa nchi zote huru kuchukua msimamo wa wazi na thabiti katika kulaani uhalifu wa wavamizi dhidi ya taifa la Iran.

Araghchi, amefafanua kuhusu matukio ya hivi karibuni katika eneo la Asia Magharibi na amekumbusha kuwa vita hivi vimeanzishwa na kulazimishwa kwa Iran na eneo zima na Marekani pamoja na utawala wa Kizayuni wa Israel unaokalia kwa mabavu ardhi za Palestina, na kwamba Iran kwa sasa inajihami kulinda mamlaka yake ya kitaifa, usalama wa taifa na ukamilifu wa mipaka yake.

Akirejelea uvamizi wa kijeshi wa Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran kama chanzo kikuu cha ukosefu wa usalama katika eneo la Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormuz, Araghchi amesisitiza kuwa hatua ya Iran ya kuzuia kupita kwa vyombo vya majini vinavyohusiana na wavamizi inazingatia sheria za kimataifa na inalenga kulinda usalama wa taifa wa Iran dhidi ya mashambulizi haramu ya wavamizi. Hata hivyo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa mtazamo wa uwajibikaji, imeweka pia utaratibu wa kuwezesha upitaji salama wa meli zisizo na uhasama kupitia uratibu na mamlaka husika za Iran.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, amesisitiza misimamo ya kimsingi ya nchi yake ya kulaani matumizi ya nguvu na kusisitiza heshima kwa mamlaka ya kitaifa na ukamilifu wa mipaka ya nchi, alisisitiza umuhimu wa kutafuta njia za haki za kumaliza vita na kurejesha amani na uthabiti katika eneo hilo.

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Afrika Kusini pia walikubaliana kuendeleza mashauriano kati ya maafisa wa nchi hizo mbili kuhusu masuala ya kisiasa, kiuchumi na ya kikanda.