Kenyatta: Vikosi vya AMISOM vimepiga hatua katika mapambano dhidi ya Al-Shabab
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i13792-kenyatta_vikosi_vya_amisom_vimepiga_hatua_katika_mapambano_dhidi_ya_al_shabab
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema jeshi la Somalia na vikosi vya Umoja wa Afrika vilivyotumwa nchini humo (AMISOM) vimepiga hatua ya kuridhisha katika vita dhidi ya wanamgambo wa kundi la Al-AShabab nchini Somalia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 23, 2016 00:20 UTC
  • Kenyatta: Vikosi vya AMISOM vimepiga hatua katika mapambano dhidi ya Al-Shabab

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema jeshi la Somalia na vikosi vya Umoja wa Afrika vilivyotumwa nchini humo (AMISOM) vimepiga hatua ya kuridhisha katika vita dhidi ya wanamgambo wa kundi la Al-AShabab nchini Somalia.

Rais wa Kenya ameyasema hayo Ikulu ya Nairobi katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry na kusisitiza kwamba sambamba na kuondolewa hatua kwa hatua askari wa Kenya walioko nchini Somalia ndani ya kipindi cha miaka miwili kuna umuhimu pia wa kuimarishwa uwezo wa jeshi la taifa la nchi hiyo ili liweze kushika hatamu za kutekeleza majukumu.

Baada ya mazungumzo ya muda wa saa mbili aliyofanya na Rais wa Kenya hapo jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani aliungana na mawaziri wa mambo ya nje wa Kenya, Somalia, Sudan ya Kusini, Sudan na Uganda ili kujadili machaguo yanayohusiana na utekelezaji wa mchakato wa kurejesha amani nchini Sudan Kusini.

Kikao cha Kerry na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Mashariki mwa Afrika

Mawaziri wa mambo ya nje wa Djibouti na Tanzania nao pia walihudhuria kikao hicho.

Hayo yanajiri huku madola makubwa duniani yakishirikiana na nchi za kanda ya Mashariki mwa Afrika yakijaribu kutoa mashinikizo kwa pande zinazopigana nchini Sudan Kusini mbali na vikwazo walivyowekewa baadhi ya viongozi wa nchi hiyo.

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na hasimu wake wa kisiasa Riek Machar

Moja ya ajenda zilizojadiliwa katika kikao hicho cha jana ni mpango wa Umoja wa Mataifa wa kupelekwa askari 4,000 katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba katika kutoa msukumo kwa vikosi vya kulinda amani vya umoja huo vilivyoko nchini humo.

Umoja wa Mataifa umeitishia serikali ya Juba kuwa endapo haitatoa ushirikiano kwa mpango wa kutumwa askari 4,000 wa kulinda amani huko mjini Juba itawekewa vikwazo vya silaha.../