Kerry aitaka Sudan Kusini kuheshimu makubaliano ya amani
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani amewataka viongozi wa Sudan Kusini kufungamana na makubaliano ya amani ya nchi hiyo.
John Kerry amewataka viongozi wa jeshi la Sudan Kusini kutekeleza kikamilifu vipengee vya makubaliano ya amani, kinyume na hivyo watakabiliwa na vikwazo na adhabu kutoka Umoja wa Mataifa.
John Kerry ameongeza kuwa serikali na wananchi ndio wanaopasa kusimamia mchakato wa kusaka amani na kutekeleza ahadi zilizotolewa ndani ya makubaliano hayo.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani ameashiria kutumwa kikosi cha kulinda amani cha kimataifa barani Afrika na kusema kuwa wanajeshi hao si vikosi vya uingiliaji kati ambao watautia hatarini uwezo na mamlaka ya kujitawala ya Sudan Kusini, bali jukumu kuu la wanajeshi hao ni kuwalinda raia na mali zao huko Juba mji mkuu wa Sudan Kusini.
John Kerry ametoa tahadhari hiyo kufuatia kufanyika vikao hapo jana huko Nairobi mji mkuu wa Kenya kati yake na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Somalia, Sudan Kusini na Sudan. Pande hizo zilizungumzia kuhusu kuongezeka machafuko huko Sudan Kusini na suala la kutuma askari jeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa huko Juba.
Mapigano ya miezi kadhaa iliyopita huko Juba mji mkuu wa Sudan Kusini yamezidisha wasiwasi kuhusu uwezekano wa kutokea vita vya ndani nchini humo.