Mgomo wa sekta ya uchukuzi Kenya waahirishwa kuruhusu mazungumzo baina ya serikali na sekta hiyo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i138472-mgomo_wa_sekta_ya_uchukuzi_kenya_waahirishwa_kuruhusu_mazungumzo_baina_ya_serikali_na_sekta_hiyo
Mgomo wa sekta ya uchukuzi uliokuwa umeingia siku ya pili nchini Kenya umeahirishwa kwa muda wa siku saba ili kutoa nafasi kwa mazungumzo kati ya serikali na viongozi wa sekta hiyo.
(last modified 2026-05-19T11:05:44+00:00 )
May 19, 2026 11:02 UTC
  • Mgomo wa sekta ya uchukuzi Kenya waahirishwa
    Mgomo wa sekta ya uchukuzi Kenya waahirishwa

Mgomo wa sekta ya uchukuzi uliokuwa umeingia siku ya pili nchini Kenya umeahirishwa kwa muda wa siku saba ili kutoa nafasi kwa mazungumzo kati ya serikali na viongozi wa sekta hiyo.

Maandamano na migomo ya kupinga kupanda kwa bei ya mafuta yaliibuka katika miji kadhaa nchini Kenya jana Jumatatu huku athari mbaya za vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran zikiendelea kuhisika duniani kote.

Muungano wa Sekta ya Uchukuzi Kenya ulitangaza Jumapili kuwa magari yote yatasitisha huduma kuanzia saa sita usiku wa kuamkia Jumatatu, kama ishara ya kupinga ongezeko la sasa la bei za mafuta.

Tangazo la kuahirishwa mgomo wa sekta ya uchukuzi limetolewa na Waziri wa Uchukuzi wa Kenya, Kipchumba Murkomen baada ya mkutano na viongozi wa sekta hiyo uliohudhuriwa pia na Waziri wa Kawi, Opiyo Wandayi.

Bw Murkomen amesema serikali imekubaliana na viongozi hao kuendelea na mazungumzo katika ngazi za juu ili kutafuta suluhu ya malalamishi yaliyoibuliwa na wadau wa uchukuzi.

Hata hivyo, viongozi wa sekta hiyo wameonya kuwa mgomo huo unaweza kurejea baada ya siku saba iwapo serikali haitazingatia matakwa yao.

Mgomo huo uliokuwa umeathiri shughuli za usafiri katika maeneo mbalimbali nchini ulianzishwa kupinga kupanda bei ya mafuta na gharama nyingine za uendeshaji katika sekta ya uchukuzi.

Mamlaka ya Usimamizi wa Nishati na Petroli ya Kenya (EPRA) wiki iliyopita ilipandisha bei ya rejareja ya mafuta kwa asilimia 23.5—hatua iliyofuatia ongezeko jingine la asilimia 24.2 mwezi uliopita.

Kupanda kwa gharama za mafuta sasa kunasukuma juu bei za chakula na bidhaa nyingine muhimu.

Mapema, vyombo vya habari viliripoti kuwa takribani watu wanne wameuawa na wengine 30 kujeruhiwa nchini Kenya wakati maandamano ya kitaifa yakizuka kupinga kupanda kwa kasi kwa bei ya mafuta.

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani Kipchumba Murkomen, watu wengine wasiopungua 348 walikamatwa siku ya Jumatatu, wakati wananchi walipokusanyika mitaani kuunga mkono mgomo wa usafiri wa umma uliotangazwa kitaifa.

Katibu Mkuu wa chama tawala cha UDA, Hassan Omar, kwa upande wake amesema kuwa hasira ya umma haipaswi kuelekezwa kwa serikali, bali inapaswa kuelekezwa kwa tawala za Marekani na Israel, ambazo ndizo zilizoanzisha vita dhidi ya Iran, hali ambayo imesababisha kuyumba kwa usambazaji wa mafuta duniani.