Nabih Berri: Kwa pamoja tutaikomboa na kuijenga upya Lebanon
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i138628-nabih_berri_kwa_pamoja_tutaikomboa_na_kuijenga_upya_lebanon
Katika siku ya kumbukumbu ya kukombolewa Lebanon kutoka kwenye makucha ya utawala ghasibu wa Israel, Nabih Berri, Spika wa Bunge la nchi hiyo amesema kuwa, adui Mzayuni hatasita hata kidogo kulipiza kisasi dhidi ya Lebanon na kuongeza kwamba kwa pamoja watu wa nchi hiyo wana uwezo wa kuikomboa na kuijenga upya.
(last modified 2026-05-25T14:30:23+00:00 )
May 25, 2026 14:22 UTC
  • Nabih Berri
    Nabih Berri

Katika siku ya kumbukumbu ya kukombolewa Lebanon kutoka kwenye makucha ya utawala ghasibu wa Israel, Nabih Berri, Spika wa Bunge la nchi hiyo amesema kuwa, adui Mzayuni hatasita hata kidogo kulipiza kisasi dhidi ya Lebanon na kuongeza kwamba kwa pamoja watu wa nchi hiyo wana uwezo wa kuikomboa na kuijenga upya.

Katika taarifa ya kuadhimisha kumbukumbu ya ukombozi wa Lebanon, Berri amesema kuwa mwaka huu, Mei 25 unakuja wakati ambapo ardhi, watu, na maslahi ya taifa na matukufu mengine katika historia ya Lebanon yamekuwa yakihujumiwa kupitia uvamizi wa Israel kwa muda wa miaka mitatu iliyopita. Tangu Februari iliyopita, uchokozi wa utawala haramu wa Israel umechukua sura hatari ya vita vya mauaji ya halaiki na uharibifu wa makusudi unaolenga kuvuruga na kutokomeza sekta zote za miundombinu pamoja na maisha ya kawaida kusini mwa Lebanon, katika maeneo ya Bonde la Bekaa na vitongoji vya kusini mwa Beirut.

Spika wa Bunge la Labanon amesisitiza kuwa awali walikuwa wametoa tahadhari na maonyo ya lazima kuhusu tamaa na uchokozi huu wa Wazayuni katika siku za mwanzo baada ya ukombozi wa Mei 2000, na kuongeza kwamba ukombozi wa nchi na watu ulikuwa “Jihadi ndogo” ambayo gharama yake ilikuwa kafara ya juu na safi kabisa, mashahidi, waliojeruhiwa na wafungwa wa vita, na kwamba kuhifadhi na kulinda mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hicho dhidi ya wavamizi wa Kizayuni ni “jihadi kubwa zaidi.”

Licha ya kusitishwa rasmi vita katika ardhi ya Lebanon kati ya utawala wa kibaguzi wa Israel na harakati ya muqawama ya Hizbullah, lakini utawala huo umepuuzilia mbali isitishaji vita huo na kuendelea kufanya mauaji ya kinyama na ya umati dhidi ya watu wasio na hatia wa Lebanon na hasa watoto wadogo, wazee na wanawake. Hayo yote yanafanyika kwa uungaji mkono wa moja kwa moja wa Marekani na nchi nyingine za Magharibi zinazodai kutetea haki za binadamu. La kusikitisha zaidi ni kwamba hata baadhi ya nchi za Kiarabu za eneo zinashirikiana kwa njia moja au nyingine na utawala haramu wa Israel katika mauaji hayo dhidi ya ndugu zao wa Lebanon, sawa kabisa na kama ilivyoshuhudia huko nyuma kuhusiana na mauaji ya halaiki ya utawala huo dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.

Taarifa ya Nabih Berri inasema kuwa utawala wa Israel uliotimuliwa katika ardhi ya Lebanon hautasita hata kidogo kulipiza kisasi dhidi ya nchi hiyo; nchi ambayo katika vita vya ukombozi, ilitoa somo muhimu la utu, umoja na kujitolea, somo ambalo halieleweki kwa utawala wa Kizayuni ambao umebobea katika sanaa ya mauaji, uharibifu, uhamisho wa kulazimishwa, mauaji ya watoto na uvunjaji wa kila thamani ya ubinadamu na utakatifu.

Spika wa Bunge la Lebanon ameongeza kuwa Siku ya Uhuru ya mwaka huu inasadifiana na Eid al-Adha, wakati ambapo taifa la Lebanon, pamoja na makabila, rangi, mioyo na sauti zake tofauti, zinaungana katika kumtii Mwenyezi Mungu na katika umoja wa malengo.

Katika taarifa yake hiyo, Spika Berri amezungumzia uvamizi wa utawala wa Kizayuni dhidi ya matabaka na madhehebu yote ya Lebanon, na kutaka kukomeshwa chuki na fitna nchini. Pia ametoa wito kwa Walebanon wote kuwa tayari kujitolea mhanga na kusimama kidete katika kulinda ardhi na mipaka ya nchi na kukabiliana vilivyo na wavamizi wa Kizayuni.

Huku akipongeza na kuthamini vikosi vyote vya mapambano ya ukombozi, jeshi, na watu wa Lebanon wanaoilinda nchi yao kwa hali na mali, amemalizia kwa kusema kuwa kwa pamoja waliikomboa nchi yao, na kwa pamoja wanaweza kuikomboa tena na kuijenga upya.