Sudan Kusini yatakiwa kuheshimu makubaliano ya amani
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani amewata viongozi wa Sudan Kusini waheshimu na kufungamana na makubaliano ya kusaka amani ya nchi hiyo.
John Kerry Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani Jumatatu wiki hii aliwataka viongozi wa ngazi za juu wa Sudan Kusini watekeleza kikamilifu vipengee vya makubaliano ya amani, kinyume na hivyo, watakabiliwa na vikwazo na adhabu kutoka Umoja wa Mataifa.
Kerry alitoa tahadhari hiyo Jumatatu akiwa huko Nairobi mji mkuu wa Kenya katika mazungumzo kati yake na Rais Uhuru Kenyatta wa nchi hiyo, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Somalia, Sudan Kusini na Sudan. Pande hizo zilijadili kupamba moto hali ya machafuko huko Sudan Kusini na kujadili pia suala la kutumwa wanajeshi wa kulinda amani huko Juba mji mkuu wa Sudan Kusini. Matukio ya kisiasa ya hivi karibuni huko Sudan Kusini yamezidisha hali ya wasiwasi kuhusu uwezekano wa kushtadi mapigano nchini humo. Riek Machar Makamu wa zamani wa Rais wa Sudan Kusini aliondoka Juba kufuatia kujiri mapigano mwezi uliopita kati ya wafuasi wake na wa Rais Salva Kiir yaliyopelekea kuuawa na kujeruhiwa mamia ya watu. Baada ya Machar kuondoka Juba, Rais Salva Kiir alimteuwa Taban Deng kuwa Makamu wake. Taarifa iliyosema kuwa Machar amepata hifadhi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na matamshi yake kwamba atapambana na uroho wa kisiasa huko Juba, yamesababisha ghasia na msuguano kati ya wafuasi wa makundi hayo mawili makubwa ya kisiasa huko Sudan Kusini. Machar amesisitiza kuwa ataendelea kufuatilia matakwa ya kisiasa kupitia wafuasi wake huko Juba.
Baadhi ya wataalamu wa mambo wanaamini kuwa kuwepo nchini Kongo Riek Machar ni moja ya mambo yanayoshadidisha mivutano ya kisiasa nchini humo na kwamba msimamo wake huo unazidisha hofu ya kuibuka vita vingine huko Sudan Kusini.
Moja ya sababu zilizopelekea kujiri vita vya miaka kadhaa nchini humo ni uhasama wa makaila mawili makuu katika kuwania madaraka na vile vile uingilia wa siri wa serikali za nchi ajinabi katika masuala ya Sudan Kusini. Salva Kiir anatoka katika kabila la Dinka, na Riek Machar kabila la Nuer.
Baada ya pande hizo hasimu kusaini makubaliano ya kusaka amani mwezi Agosti mwaka jana na Riek Machar kuchaguliwa tena kuwa Makamu wa Rais, weledi wa mambo walitaraji kuwa, vita vingesita huko Sudan Kusini na amani kurejea. Hata hivyo kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa na kugawana madaraka kati ya Riek Machar na Salva Kiir pia kumeshindwa kuwadhaminia na kuwarejeshea raia wa nchi hiyo amani na utulivu.
Ban Ki-moon Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuwa yapo machaguo matatu yanayojumuisha vikwazo vya silaha, zuio la kusafiri na fedha dhidi ya viongozi wa kisiasa, na kutuma wanajeshi walinda amani kwa jili ya kuimarisha kikosi cha kulinda amani kilichopo Sudan Kusini chenye askari jeshi 12,000. Ripoti zinaarifu juu ya hali ya kusikitisha ya kibinadamu nchini humo. Maafa ya kibinadamu yameikumba Sudan Kusini kufuatia kuanza mapigano na kuendelea hali ya mchafukoge nchini humo.