UNICEF yaonya kuhusu lishe duni kwa watoto wa Afrika
Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umesema kuwa, kuna watoto milioni moja wana lishe duni barani Afrika
Gazeti la Le Monde la nchini Ufaransa limeinukuu UNICEF ikisema hayo jana (Jumatano) katika ripoti yake kuhusiana na ukame mkali katika maeneo ya mashariki na kusini mwa bara la Afrika na kusema kuwa, karibu watoto milioni moja wa maeneo hayo wako katika hatari ya kukumbwa na janga kubwa la lishe duni.
Leila Gharagozloo-Pakkala, mkurugenzi wa UNICEF barani Afrika amesema, mabadiliko ya hali ya hewa yamepelekea kutokea hali hiyo na kwamba watoto wadogo ndio watakaodhurika zaidi iwapo ukame utaendelea kwenye maeneo hayo.
Kwa upande wake shirika la kimataifa la masuala ya chakula FAO limetangaza kuwa, utabiri wa hali ya hewa unaonesha kuwa, mvua zitaendelea kupungua kunyesha kwenye maeneo hayo hadi mwezi Machi mwaka huu.
Limesema watu milioni 49 wamekumbwa na wimbi la ukame huko kusini mwa bara la Afrika.
Nchi za Malawi, Madagascar na Zimbabwe ndizo zilizoathiriwa zaidi ya janga la ukame.