Wajumbe wa Baraza la Usalama la UN wako Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i14533-wajumbe_wa_baraza_la_usalama_la_un_wako_sudan_kusini
Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamewasili Juba, Sudan Kusini tayari kwa ziara ya siku tatu katika nchi hiyo inayokumbwa na machafuko ya ndani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 03, 2016 02:31 UTC
  • Wajumbe wa  Baraza la Usalama la UN wako  Sudan Kusini

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamewasili Juba, Sudan Kusini tayari kwa ziara ya siku tatu katika nchi hiyo inayokumbwa na machafuko ya ndani.

Taarifa ya Umoja wa Mataifa inasema wajumbe hao watatathmini kile kinachoelezwa kuwa ni janga la kibinadamu la kusikitisha.

Samantha Power, mwakilishi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa amezungumza na wanahabari baada ya kuwasili Juba na kusema ujumbe huo uko Juba kutokana na wasiwasi  kuhusu mapigano ambayo yamezidi kuzorotesha hali ya usalama na pia kuongeza hali mbaya ya kibinadamu kwa raia wa nchi hiyo.

Amesema  Baraza la Usalama hupokea ripoti za kusikitisha za vikwazo vinavyowekwa ili kukwamisha utendaji wa kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini humo, UNMISS,  na watoa huduma za misaada.

Wajumbe wa Baraza la Usalama la UN wakiwasili Juba, 2,9,2016

 

Ujumbe huo unatazamiwa kufahamisha pande zote zinazozozana kuwa ni muhimu sana kuacha Umoja wa Mataifa  ufanye kazi zake.

Pamoja na kuongeza muda wa UNMISS, Baraza la Usalama pia limeafiki kupelekwa kwa kikosi cha kimataifa ambacho kimeruhusiwa kutumia nguvu kulinda mali za Umoja wa Mataifa, raia, na wafanyakazi wanaotoa huduma za kibinadamu.

Kuongezeka mapigano Sudan Kusini kumezidisha wasiwasi kuhusu uwezekano wa kutokea vita vya ndani na kuulazimu Umoja wa Mataifa kutuma wanajeshi zaidi nchini humo.

Baada ya kuzuka mapigano makali ya umwagaji damu baina ya wafuasi wa Riek Machar na wale wa Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini mjini Juba kuanzia tarehe 8 hadi 11 mwezi uliopita wa Julai, Riek Machar aliondoka Juba na kukimbilia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Imedokezwa kuwa hivi sasa Machar yuko Khartoum, nchini Sudan akipokea matibabu.