Viongozi wa kidini Sudan Kusini wataka kutumwa wanajeshi Juba
Viongozi wa kidini huko Sudan Kusini wametaka kutumwa vikosi vya jeshi katika mji mkuu wa nchi hiyo, Juba.
Viongozi hao wametaka kufanyike jitihada za kumshawishi Rais Salva Kiir wa nchi hiyo ili aafiki suala la kutumwa nchini humo kikosi cha askari jeshi wa kulinda amani katika maeneo yaliyoathiriwa na mapigano katika mji mkuu wa nchi hiyo Juba. Waliyaeleza hayo jana kwenye kikao cha mabalozi 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa huko Juba.
Serikali ya Sudan Kusini imepinga suala la kutumwa nchini humo wanajeshi zaidi wa kulinda amani. Wimbi jipya la mapigano liliibuka huko Sudan Kusini mwezi Julai mwaka huu wakati vikosi vya askari wanaomuunga mkono rais Salva Kiir vilipigana na wanamgambo watiifu kwa Riek Machar, Makamu wa zamani wa rais wa nchi hiyo.
Kushtadi hali ya mchafukoge huko Sudan Kusini kunatishia makubaliano ya amani yanayolegalega ambayo yalitiwa saini mwaka uliopita kuhitimisha vita vya ndani vya miezi 18 nchini humo. Raia wa Sudan Kusini karibu milioni nne na laki nane ambao ni karibu nusu ya jamii ya nchi hiyo wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa machafuko na vitendo vya kubakwa wanawake vinavyofanywa na makundi ya wahalifu na kuchomwa moto vijiji vimeongezeka nchini Sudan Kusini, mbali na kuuawa makumi ya maelfu ya watu kwenye mapigano huko Sudan Kusini.