Wanajeshi Nigeria wanawauzia silaha magaidi wa Boko Haram
Imebainika kuwa baadhi ya wanajeshi fisadi nchini Nigeria wanawauzia silaha magaidi wa kundi la kitakfiri la Boko Haram.
Kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa Jumapili na Shirika la Associated Press, maafisa kadhaa wa ngazi za juu nchini Nigeria wanachunguzwa kwa siri baada ya kugundulika kuwa wamekuwa wakiwauzia silaha magaidi wa Boko Haram.
Afisa wa ngazi za juu katika jeshi la Nigeria amethibitisha kuwa baadhi ya wanajeshi wanawauzia silaha Boko Haram katika kile alichokitaja kuwa ni usaliti kwa Wanigeria. Meja Jenerali Lucky Irabor, kamanda wa oparesheni kaskazini mashariki mwa Nigeria amebaini kuwepo usaliti huo pasina kutoa maelezo zaidi.
Afisa mwingine wa jeshi ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema kamanda wa brigedi ni kati ya maafisa wa kijeshi ambao wamefikishwa kizimbani kujibu mashtaka kuhusu ufisadi katika vita dhidi ya magaidi wa Boko Haram.
Duru zinaarifu kuwa Jenerali Alex Badeh aliyekuwa wakati mmoja mkuu wa Jeshi la Nigeria ni kati ya washukiwa wa ubadhirifu wa fedha zilizokuwa zimetengewa vita dhidi ya Boko Haram. Anaripotiwa kuiba dola milioni 24 na kujenga jengo kubwa la kibiashara katika mji mkuu Abuja. Mkuu wa sasa Jeshi la Nigeria Luteni Jenerali Tukur Buratai pia yuko chini ya mashinikizo baada ya kubainika kuwa amenunua nyumba mbili zenye thamani ya dola milioni moja na nusu huko Dubai.
Zaidi ya watu 20,000 wameuawa tokea magaidi wa Boko Haram walipoanzisha jinai zao kaskazini mwa Nigeria na baadhi ya nchi jirani.