MONUSCO: Kuna maelfu ya wakimbizi wa Sudan Kusini katika ardhi ya DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i14926-monusco_kuna_maelfu_ya_wakimbizi_wa_sudan_kusini_katika_ardhi_ya_drc
Kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (MONUSCO) kimetangaza kuwa, kuna maelfu ya wakimbizi wa Sudan Kusini waliokimbilia nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 08, 2016 23:10 UTC
  • MONUSCO: Kuna maelfu ya wakimbizi wa Sudan Kusini katika ardhi ya DRC

Kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (MONUSCO) kimetangaza kuwa, kuna maelfu ya wakimbizi wa Sudan Kusini waliokimbilia nchini humo.

Taarifa ya MONUSCO imeeleza kuwa, wakimbizi takribani elfu 20 kutoka Sudan Kusini wamekimbilia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hususan katika Jimbo la Orientale huko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. 

Félix Prosper Basse, msemaji wa kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (MONUSCO)  amesema kuwa, raia hao wa Sudan Kusini wameomba hifadhi Congo DRC wakikimbia machafuko katika nchi yao.

Maisha magumu ya wakimbizi wa Sudan Kusini

Imeelezwa kuwa, wakimbizi hao kutoka Sudan Kusini wanakabiliwa na hali mbaya na wanahitajia misaada ya haraka ya kibinadamu.

Mapigano mapya baina ya wafuasi wa Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na aliyekuwa makamu wake Riek Machar mjini Juba yaliibuka mwezi Julai mwaka huu na kupelekea zaidi ya watu 300 kuuawa na maelfu ya wengine kuyakimbia makazi yao. Baadhi ya duru za habari zinasema idadi ya waliouawa katika mapigano hayo yumkini imepindukia watu 1,000.

Hitilafu za kisiasa na kikabila zinatajwa kuwa sababu kuu za mapigano na mivutano ya mara kwa mara kati ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka na hasimu wake, Machar anayetoka kabila la Nuer.