Kiir, Machar wajitajirisha huku vita vikiendelea Sudan Kusini
Wanasiasa wa Sudan Kusini wamepata utajiri wa mamilioni ya dola wakiwa pamoja na familia zao huku raia wa kawaida wakiendelea kupoteza maisha na kupata masaibu kutokana na kuendelea vita na njaa nchini humo.
Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la kutetea haki la The Sentry, mahasimu wawili wa kisiasa Sudan Kusini, yaani Rais Salva Kiir na Riek Machar hasimu wake mkuu aliyetimuliwa kutoka nafasi ya makamu wa rais wamejikusanyia idadi kubwa ya fedha. Ripoti hiyo imesema wanasiasa wengi wa Sudan Kusini wana akaunti katika benki za nchi jirani ya Kenya.
Aidha Rais Kiir na mpizani wake Machar wana nyumba za kifahari zinazokaribiana katika mtaa wa matajiri wa Lavington mjini Nairobi. Ripoti hiyo ya kurasa 65 inasema wajukuu wa Salva Kiir wanasoma katika shule binafsi mjini Nairobi ambapo karo ya kila mtoto mmoja ni dola elfu kumi kwa mwaka.
Aidha wanafamilia wa Kiir na Machar huonekana nchini Kenya wakistarehe wakiwa katika hoteli ghali zaidi na wakiendesha magari ya kifahari. Hii ni katika hali ambayo vita vya ndani nchini Sudan Kusini vimepelekea raia milioni 1.6 kati ya milioni 12 nchni kukimbia makaazi yao na kuishi katika kambi za wakimbizi wa ndani au katika nchi jirani.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa raia milioni 5.2 wa Sudan Kusini wanahitaji misaada ya dharura. Serikali ya Sudan Kusini imekiri kuwa dola bilioni nne fedha za serikali zimeibiwa na maafisa wa sasa na wa zamani serikalini.
Ripoti ya The Sentry inasema wanasiasa wa Sudan Kusini wanawagonganisha wananchi wa makabila tafauti huku wao binafsi wakiendelea kutajirika kutokana na vita nchini humo.