Somalia na changamoto ya kurejea nyumbani wakimbizi walioke nje ya nchi
Katika hali ambayo vita vya ndani na mizozo ya kikabila inayoendelea sasa katika nchi kadhaa za Kiafrika vimeibua wimbi kubwa la wakimbizi katika nchi jirani za maeneo mbalimbali ya bara hilo, serikali za nchi za bara hilo sasa zinakabiliwa na matatizo mapya ya jinsi ya kurejea wakimbizi hao katika nchi zao baada ya kumalizika vita na machafuko ya ndani katika baadhi ya nchi hizo.
Somalia hivi sasa huwenda ikawa ni mfano mzuri wa hali hiyo. Mchakato wa kurejea wakimbizi wa nchi hiyo kutoka katika kambi za Kenya baada ya kurejea amani na utulivu wa kiwango fulani huko Somalia, tayari umeanza. Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limekosoa mchakato wa kurejea wakimbizi wa Kisomalia kutoka Kenya likisema wakimbizi hao wanalazimika kuondoka katika kambi kubwa zaidi ya wakimbizi ya Dadaab wakiwa chini ya mashinikizo na vitisho bila ya kujua hatima ya mustakbali wao huko Somalia.
Kambi ya wakimbizi ya Dadaab iliasisiwa kaskazini mashariki mwa Kenya mwaka 1992 kwa lengo la kuwapa hifadhi raia wa Somalia ambao walikuwa wakikimbia vita vya ndani na machafuko nchini humo. Kambi hiyo kubwa ambayo ni makazi ya karibu wakimbizi laki sita, ndiyo kubwa zaidi ya wakimbizi duniani. Itakumbukwa kuwa serikali ya Kenya mwezi Juni mwaka huu ilitishia kuzifunga kambi za Dadaab na ile ya Kakuma. Uamuzi huo wa serikali ya Kenya umekabiliwa na upinzani mkubwa kutoka wa viongozi wa Somalia na baadhi ya mashirika ya kutetea haki za binadamu.
Japokuwa Umoja wa Mataifa na baadhi ya taasisi za kimataifa kama Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka zimetoa radiamali yao kwa suala hilo, lakini viongozi wa Kenya wametoa sababu zenye mashiko za kufunga kambi hizo za wakimbizi na kuwarejesha makwao wakimbizi Kisomali. Viongozi wa Kenya wanaamini kuwa, kambi za Dadaab na Kakuma zimegeuka na kuwa maficho salama ya wanamgambo wa kundi lenye misimamo ya kufurutu ada wa al Shabab lenye lengo la kuing'oa madarakani serikali kuu ya Mogadishu. Kundi la al Shabab ambalo ni tawi la mtandao wa kigaidi wa al Qaida katika eneo la Pembe ya Afrika, limefanya mashambulizi ya kigaidi katika nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) kama Kenya na Uganda, ambazo zinashirikiana na kikosi cha kulinda amani cha AMISOM na jeshi la Somalia katika kuwaangamiza wanamgambo wa kundi hilo. Shambulio na utekaji nyara uliofanywa na al Shabab katika Chuo Kikuu cha Garissa kusini mwa Kenya mwanzoni mwaka jana wa 2015 lilisababisha vifo vya wanachuo 148.
Weledi wa mambo wanaamini kuwa, vitisho vya mara kwa mara vya serikali ya Kenya kwamba itaifunga kambi kubwa ya wakimbizi ya Dadaab na kuwarejeshwa makwao wakimbizi wanaoishi kwenye kambi hiyo, vinahusiana moja kwa moja na mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa na kundi la al Shabab huko Garissa na lile la kabla yake katika kituo cha kibiashara cha Westgate jijini Nairobi. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa vitisho vya serikali ya Kenya vya kutaka kuzifunga kambi zilizoko nchini humo ni wenzo wa kisiasa unaotumiwa na nchi hiyo ili kujipatia misaada zaidi ya kifedha kutoka kwa wafadhili wa kimataifa.
Alaa kulli hal, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Joseph Nkaisssery amesisitiza kwamba idadi ya wakimbizi wanaoishi katika kambi za Dadaab na Kakuma itafikia nusu hadi mwishoni mwa mwaka huu. Kwa msingi huo, wakimbizi wa Kisomali wasiopungua laki tatu watakuwa wamerejea nchini kwao kufikia mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka huu. Operesheni ya kuwarejesha nyumbani wakimbizi hao kutoka Kenya ilianza tarehe 9 mwezi huu.