UN yatahadharisha kuhusu hatari ya mauaji ya kimbari Burundi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i15793-un_yatahadharisha_kuhusu_hatari_ya_mauaji_ya_kimbari_burundi
Kundi la wachunguzi wa Umoja wa Mataifa limetahadharisha kuhusu hatari ya mauaji ya kimbari yanayonukia huko Burundi na kueleza kuwa, mwenendo jumla wa kauli zenye kuleta mgawanyiko wa kikabila zinazotolewa na serikali ya nchi hiyo zinamaanisha kuwa mzozo unaweza kuenea hadi katika nchi nyingine za Kiafrika.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Sep 21, 2016 10:38 UTC
  • UN yatahadharisha kuhusu hatari ya mauaji ya kimbari Burundi

Kundi la wachunguzi wa Umoja wa Mataifa limetahadharisha kuhusu hatari ya mauaji ya kimbari yanayonukia huko Burundi na kueleza kuwa, mwenendo jumla wa kauli zenye kuleta mgawanyiko wa kikabila zinazotolewa na serikali ya nchi hiyo zinamaanisha kuwa mzozo unaweza kuenea hadi katika nchi nyingine za Kiafrika.

 Ripoti iliyotolewa na wataalamu watatu wa kujitegemea wa Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa, hatari ya kujiri jinai ya mauaji ya kimbari huko Burundi ni kubwa na kwamba baadhi ya ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu umejiri na unaendelea kufanyika nchini humo. Jopo hilo la wachunguzi wa kujitegemea wa Umoja wa Mataifa limeongeza kuwa ukiukaji huo wa haki za binadamu kimsingi umetekelezwa na vyombo vya serikali na wale wote wenye mfungamano na vyombo hivyo.

Itakumbukwa kuwa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mwezi Januari mwaka huu liliwaagiza wataalamu hao watatu kuchunguza kesi za ukiukaji wa haki za binadamu nchini Burundi, miezi minane baada ya kutokea machafuko nchini humo kufuatia uamuzi wa Rais Pierre Nkurunziza wa kugombea kiti cha urais kwa muhula wa tatu. Nkurunziza alishinda uchaguzi wa Rais uliofanyika mwezi Julai licha ya kupingwa vikali na wapinzani na kuibuka ghasia za mitaani za wananchi.

Askari polisi wa Burundi wakikabiliana kwa mabavu na waandamanaji

Jopo la wataalamu watatu wa kujitegemea la Umoja wa Mataifa limethibitisha katika uchunguzi wao huo kuwa, watu wasiopungua 100 waliuawa na wengine 564 kunyongwa kati ya Aprili 26 mwaka jana na Agosti 30 mwaka huu, na kuongeza kuwa vitendo vya kuwatesa raia, udhalilishaji wa kijinsia na kuwakamata kiholela vimejiri pakubwa huko Burundi.