Rais Jacob Zuma: Afrika Kusini imeazimia kufikia ustawi wa kudumu
Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini amesema kuwa, nchi yake imeazimia kufikia malengo ya ustawi wa kudumu.
Rais Zuma amesema hayo katika hotuba yake kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani na kusisitiza kwamba, nchi yake imeandaa mipango madhubuti ya kupambana na umasikini, ukosefu wa ajira na kutokuweko usawa wa kijamii.
Rais Zuma amesema kuwa, katika kipindi cha muongo mmoja uliopitya, Afrika Kusini imepiga hatua kubwa katika njia ya kutokomeza mambo ambayo ni sumu ya kufikia ustawi na maendeleo.
Rais wa Afrika Kusini ameashiria mwenendo wa kuzifanya nchi kuwa za viwanda kwamba, ni mkakati katika njia ya ustawi wa Afrika, kupambana na umasikini katika bara hilo na kuongeza kuwa, kuzifanya nchi kuwa za viwanda ni hatua ambayo inaweza kusambaratisha umasikini, ukosefu wa ajira na hata ukosefu wa usawa wa kijamii na hivyo kufungua njia ya ustawi na maendeleo.
Licha ya Afrika Kusini kutajwa kuwa imechukua hatua muhimu za kimaendeleo katika miaka ya hivi karibuni, lakini imekuwa ikikabiliwa pia na ukosefu wa ajira pamoja na kutawaliwa na ufisadi mkubwa serikalii, jambo ambalo limeifanya serikali ya Rais Jacob Zuma kukabiliwa na ukosoaji mkubwa na hata kupungua uungaji mkono wa wananchi kwa chama tawala cha nchi hiyo ANC.