Tangazo la vita la Riek Machar dhidi ya serikali ya Sudan Kusini
Makamu wa zamani wa Rais wa Sudan Kusini amesema kuwa, makubaliano ya amani na serikali ya Rais Salva Kiir hayana itibari yoyote na hivyo amewataka wafuasi wake kuanzisha vita upya.
Riek Machar, kiongozi wa waasi na makamu wa zamani wa rais nchini humo ameyasema hayo Jumapili ya jana ambapo sambamba na kutoa taarifa ya kuanzisha vita dhidi ya serikali amesisistiza kuwa, makubaliano hayo ya amani yaliyofikiwa kwa msaada wa jamii ya kimataifa, hayana itibari tena. Machar ameyasema hayo akiwa Khartoum, mji mkuu wa Sudan ambako alikimbilia baada ya kuibuka machafuko ya mwezi Julai mwaka huu huko Juba mji mkuu wa Sudan Kusini.
Katika taarifa hiyo, Machar ametangaza pia azma yake ya kuanzisha mapambano ya silaha dhidi ya utawala wa Rais Kiir kwa lengo la kile alichokisema kuwa ni kufikiwa amani, demokrasia na uhuru kamili wa Sudan Kusini. Wakati huo huo, James Wani Igga Makamu wa Rais wa Sudan Kusini amesema kuwa, ana matumaini serikali ya Juba ikipata uungaji mkono wa wananchi pamoja na uaminifu wao kwa serikali hiyo, itaweza kurejesha amani na utulivu wa kudumu katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.
Afisa huyo wa serikali ya Sudan Kusini amewataka pia wananchi wa nchi hiyo kuwa na uvumilivu. Ni miezi kadhaa sasa ambapo vita vinaendelea nchini Sudan Kusini. Licha ya kwamba kutiwa saini makubaliano ya amani mwaka jana kulileta matumaini ya kurejea amani na utulivu katika nchi hiyo, lakini katika kipindi hicho hicho baada ya kutiwa saini makubaliano hayo, kuna wataalamu wa mambo ambao waliyatilia shaka makubaliano hayo. Ugawanaji wa madaraka kufuatia kuzidi kuwa mbaya hali ya kibinadamu huko Sudan Kusini kwa upande mmoja na suala la kuwekewa vikwazo nchi hiyo kwa upande wa pili ndiyo mambo yaliyowalazimisha Riek Machar na Rais Salva Kiir wakubali shingo upande kutekeleza makubaliano hayo. Baada ya kutekelezwa ugawanaji madaraka akthari ya wananchi, mataifa, viongozi na asasi za kieneo na kimataifa zilipata matumaini kwamba, uhasama na vita vitafikia tamati nchini humo. Hta hivyo machafuko ya umwagaji damu yalizuka ghafla mwezi Julai kati ya vikosi vitiifu kwa Rais Salva Kiir na vile vya Riek Machar na kuubadilisha kabisa mkondo wa kisiasa wa nchi hiyo.
Kuondoka Juba Machar na kuainishwa mtu mwingine kushika wadhifa wa Makamu wa Rais kwa mara nyingine tena kulimpa matumaini Rais Salva Kiir ya kurejea amani nchini humo kiasi kwamba, juma lililopita Kuol Manyang Juuk Waziri wa Ulinzi wa Sudan Kusini pamoja na Akuei Bona Malwal mwakilishi wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa walitangaza kwamba, utulivu wa kiwango fulani umerejea nchini humo na kwamba hata Bunge la Taifa limeanza shuhughuli zake. Pamoja nahyo, wataalamu wa mambo wanasema kuwa, kuna ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu nchini Sudan Kusini huku vitisho, kamata kamata pamoja na vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya raia, navyo vikiendelea. Filhali, hali ya mambo Sudan Kusini imevurugika zaidi na hivyo kuzusha wasiwasi wa kutokea tena vita vya ndani, hasa baada ya Riek Machar kutangaza vita dhidi ya serikali ya Juba.
Baadhi ya wajuzi wa mambo wanaamini kuwa, moja ya sababu zilizopelekea kujiri vita vya miaka kadhaa nchini humo ni uhasama wa kuwania madaraka baina ya makabila mawili makuu na vile vile uingiliaji wa siri wa madola ya Magharibi katika masuala ya ndani ya Sudan Kusini. Hapana shaka kuwa, endapo tangazo la vita la Riek Machar litafanyiwa kazi, hakutakuwa na matokeo mengine ghairi ya mauaji na kushadidi umasikini. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana asasi za kieneo zikasisitizia wajibu wa kufanyika mazungumzo ya kisiasa kwa ajili ya kuzuia kuzuka tena vita nchini humo.