Kushtadi mateso dhidi ya wafungwa wa kisiasa Misri
Watetezi wa haki za binadamu jana walibainisha wasiwasi wao katika ripoti waliyotoa kuhusu hali mbaya waliyonayo wafungwa wa kisiasa huko Misri, khususan wale waliopo katika jela ya Aqrab huko Cairo mji mkuu wa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wafanyakazi wa jela ya Aqrab wanaamiliana vibaya kwa kuwapiga na kuwatesa wafungwa katika jela hiyo sambamba na kuwaweka wafungwa katika seli ndogo sana za mtu mmoja mmoja. Ripoti zinaeleza kuwa wafungwa nchini Misri hivi wana hali mbaya sana ikilinganishwa na kabla ya kujiri mapinduzi dhidi ya Rais halali wa nchi hiyo aliyepinduliwa Mohamed Morsi; huku haki za binadamu zikikiukwa kila uchao ndani ya jela hizo. Takwimu za Taasisi za Kutetea Haki za Binadamu zinaonyesha kuwa, idadi ya wafungwa wa kisiasa huko Misri imefika zaidi ya elfu 40 baada ya mapinduzi ya mwezi Julai mwaka 2013 dhidi ya serikali ya Mohamed Morsi Rais wa kwanza wa Misri kuwahi kuchaguliwa kwa njia ya kidemokrasia nchini humo. Hii ni katika hali ambayo serikali ya Rais wa sasa wa Misri Abdel Fattah al Sisi imezigeuza jela za nchi hiyo kuwa sehemu ya kuwaulia wafungwa wa kisiasa. Hadi sasa wafungwa zaidi ya 140 wameuawa katika jela za Misri tangu kuingia madarakani Abdel Fattah al Sisi mwezi Juni mwaka 2014. Kuuliwa wafungwa hao wa kisiasa huko Misri si ukiukaji pekee wa haki za binadamu unaotekelezwa katika jela za nchi hiyo, bali ukosefu wa suhula za afya, hali mbaya waliyonayo wafungwa, mateso wanayopata na kuzuiwa wafungwa hao kuonana na familia zao, ni katika ukiukaji mwingine wa haki za binadamu unaojiri katika jela hizo.
Al Sisi baada ya kushika hatamu za uongozi alitoa ahadi imbalimbali kwa wananchi kuhusu kuleta demokrasia nchini, hata hivyo kama wapinzani wanavyosema, rais huyo hajafanya lolote la maana ghairi ya kuwapandisha kizimbani wafungwa wa kisiasa, kuasisi utawala wa kipolisi, kuwakandamiza pakubwa wapinzani na kukiuka haki za binadamu nchini humo.
Hii ni katika hali ambayo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imetangaza habari kuhusu uanachama wa nchi hiyo katika Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa kuanzia mwaka 2017 hadi 2021. Misri itakuwa mwanachama katika kamati hiyo iliyotajwa huku taasisi za kimataifa zikiwa tayari zimelaani mara kadhaa ukandamizaji uliofanywa na serikali ya Rais Abdel Fattah al Sisi baada ya mapinduzi yaliyomuondoa madarakani Mohamed Morsi mwaka 2013. Katika fremu hiyo, kazi kubwa iliyofanywa na serikali ya Abdel Fattah al Sisi ambaye aliingia uongozini tangu Juni mwaka 2014, ni kukiuka waziwazi haki za binadamu kupitia kuwakandamiza vikali raia, kuwatia mbaroni wafanya maandamano, kuwafungulia mashtaka wapinzani kwenye mahakama zisizo za kiadilifu, kuwahukumu wapinzani vifungo vya muda mrefu jela na kuwakatia hukumu za kunyongwa na kudhibiti pakubwa vyombo vya habari huko Misri.
Hasa ikizingatiwa kuwa serikali ya Abdel Fattah al Sisi imezigeuza jela za Misri kuwa mahali pa kuwaulia wafungwa wa kisiasa. Katika mazingira kama hayo hatua ya Misri ya kupatiwa uanachama katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa nchi ambayo yenyewe inatambulika kuwa miongoni mwa nchi zinazokanyaga haki za binadamu imewashangaza weledi wa mambo. Kupewa uanachama nchi kama Misri katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kunaonyesha nguvu kubwa ya kisiasa inavyofanya kazi na upotoshaji wa maana na vigezo vya kisheria katika taasisi hiyo ya kutetea haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa. Hakuna shaka kuwa miamala hiyo ya upuuzaji haitakuwa na natija nyingine ghairi ya kuwachochea viongozi wa Misri kukiuka zaidi na zaidi haki za binadamu nchini humo.