Kongo DR yakosoa vikwazo ilivyowekewa na Marekani
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekosoa vikali hatua ya Marekani kuwawekea vikwazo maofisa wa ngazi za juu wa serikali ya Kinshasa, kwa shabaha ya kuathiri mwelekeo wa kisiasa wa nchi hiyo.
Bene M'Poko, Balozi wa Kongo DR nchini Afrika Kusini amesema serikali ya Kinshasa itakabiliana na hatua hiyo ya Washington na kuongeza kuwa, daima Marekani imekuwa ikitoa misimamo ya kukinzana kuhusu mielekeo tofauti ya kisiasa katika nchi mbalimbali, jambo ambalo amesema halikubaliki. Mwanadiplomasia huyo ameongeza kuwa, DRC imekuwa ikilengwa na nchi za Magharibi kutokana na utajiri wake wa rasilimali.
Tarehe 28 ya mwezi uliopita wa Septemba, Marekani ilitangaza vikwazo dhidi ya Meja Jenerali Gabriel Amisi Kumba, kamanda mwandamizi wa jeshi la nchi hiyo na Jenerali John Numbi, aliyekuwa Inspekta Jenerali wa Polisi na mshauri wa karibu wa Rais Kabila, katika hatua ya kumshinikiza Kabila aitishe uchaguzi wa kumchagua mrithi wa kiti chake mwezi ujao wa Novemba.
Tayari Rais Joseph Kabila ametangaza kuwa uchaguzi mkuu ambao ulitazamiwa kufanyika mwezi ujao sasa utafanyika Disemba mwaka 2018 na kusisitiza kuwa, zaidi ya watu milioni kumi watapoteza fursa ya kupiga kura iwapo uchaguzi hautaakhirishwa.
Wakati huo huo Corneille Nangaa, Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pia amesema kuwa uchaguzi mkuu utafanyika nchini mwezi Disemba mwaka 2018 na kwamba umesogezwa mbele kutokana na sababu za kilojistiki.