Kuendelea malalamiko na maandamano ya wananchi nchini Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i16990-kuendelea_malalamiko_na_maandamano_ya_wananchi_nchini_ethiopia
Malalamiko ya wananchi na maandamano ya wapinzani wa kisiasa wa serikali ya sasa ya Ethiopia yangali yanaendelea.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 08, 2016 09:16 UTC
  • Kuendelea malalamiko na maandamano ya wananchi nchini Ethiopia

Malalamiko ya wananchi na maandamano ya wapinzani wa kisiasa wa serikali ya sasa ya Ethiopia yangali yanaendelea.

Idadi ya watu waliouawa kwenye machafuko na ghasia za hivi karibuni huko Ethiopia imeongezeka kufuatia kuongezeka wimbi la maandamano dhidi ya serikali ya Addis Ababa na kushtadi anga ya machafuko ya kisiasa nchini humo.

Maandamano ya wananchi wa Ethiopia katika mji wa Bishoftu ulioko umbali wa kilomita 40 kusini mwa mji mkuu, Addis Ababa katika mkoa wa Oromia na katika maeneo jirani yalishadidi katika siku za hivi karibuni. Kwa sasa wapinzani wa serikali nchini Ethiopia wanapanga kufanya maandamano makubwa zaidi katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo. 

Maandamano ya Waethiopia

Ripoti zinsema kuwa, polisi wa Ethiopia wamekabiliana na waandamanaji kwa kuwanyunyizia gesi ya kutoa machozi na kwamba baadhi ya waandamanaji wamejeruhiwa kutokana na msongamano wa watu waliokuwa wameninimika katika mitaa mbalimbali. Waandamanaji wengi wamesema kuwa, mwenendo usio wa kiadilifu wa serikali ya Ethiopia kwa raia wa nchi hiyo kwa miaka miaka mingi sasa na vilevile matatatizo ya kijamii yanayowasumbua wananchi ni miongoni mwa sababu kuu zinazowafanya waandamane kupinga serikali.  

Miji mbalimbali ya Ethiopia, kwa miezi kadhaa sasa imekuwa ikitawaliwa na maandamano na malalamiko ya raia wengi wa nchi hiyo dhidi ya serikali. Kuwepo hitilafu za kikabila na kitamaduni, siasa zisizo za kiadilifu za serikali hususan katika sekta za uchumi, mipango za kukuza na kustawisha miji bila ya kuzingatia mtazamo wa wakazi asilia na makabila ya maeneo husika, kuongezeka matatizo ya kiuchumi na ukosefu wa ajira, ni miongoni mwa sababu zinazowasukuma wananchi wa Ethiopia kufanya maandamano ya kuipinga serikali.  

Wananchi wa Ethiopia wakipinga mauaji ya raia  

Maandamano ya wananchi katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika yameshtadi huku idadi ya watu waliouliwa na polisi  katika mikoa miwili ya Amhara na Oromia ikiongezeka. Viongozi wa serikali ya Addis Ababa wametangaza kuwa, watu 55 wameuwa katika machafuko ya hivi karibuni katika mji wa Bishoftu, huku wachambuzi wa mambo wakiitaja idadi ya wahanga wa tukio hilo kuwa ni zaidi ya 100.  Wakati huo huo polisi ya Ethiopia imezidisha ukandamizaji na kutumia mabavu dhidi ya raia wanaoandamana sambamba na kushika kasi malalamiko ya wananchi.

Serikali ya Ethiopia kwa upande wake imetaka kusitishwa maandamano ya mitaani na kukomeshwa ghasia zilizoikumba miji miwili nchini humo hivi karibuni.

Ethiopia ni miongoni mwa nchi kongwe za mashariki mwa bara la Afrika na inakadiriwa kuwa na jamii ya watu karibu milioni moja. Miaka ya nyuma nchi iligubikwa na vita na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kutokana na hitilafu za kikabila na kikaumu.

Mji wa Bishoftu palipojiri maandamano ya umwagaji damu huko Ethiopia 

Matukio yanayojiri sasa nchini Ethiopia yamemfanya Nkosazana Dlaimin Zuma, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika kusisitiza hivi majuzi kwamba, umoja huo unakaribisha uamuzi wa serikali ya Ethiopia wa kutaka kutambuliwa wahusika wa matukio ya kuhuzunisha katika mkoa wa Oromiya yaliyosababisha vifo vya raia wengi.

Mkoa wa Oromia ulikuwa makao makuu ya maendeleo ya kiviwanda ya Ethiopia. Hata hivyo wenyeji wa eneo hilo wanalalamikia kuporwa ardhi zao kwa ajili ya ujennzi wa viwanda na nyumba za raia . Ikijibu malalamiko ya wananchi, serikali ya Ethiopia imesema kuwa maandamano ya wananchi yaliyofanywa katika maeneo hayo ni ya kisiasa na kinyume cha sheria na kwamba itakabiliana nayo vikali.

Serikali ya Ethiopia ambayo inahesabika kuwa muitifaki wa karibu wa nchi wa Magharibi inatuhumiwa pia kuwakandamiza wapinzani na kufunga mtandao wa intaneti.

Umaskini na hali mbaya ya kiuchumi, Ethiopia

Hivi sasa kuna wasiwasi wa kutokea kushadidi zaidi machafuko ya ndani huko Ethiopia kutokana na kuendelea mwenendo wa sasa. Hii ni katika hali ambayo matatizo ya kiuchumi, ukame na hitilafu za mpaka ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazoikabili nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Kwa msingi huo inaonekana kuwa viongozi wa Ethiopia wanapasa kwanza kuzingatia matatizo ya watu wa nchi hiyo na kufanya marekebisho ya kisiasa ili kupunguza ubaguzi wa kikabila na kikaumu, na wakati huo huo itayarishe mazingira ya kuishi kwa usawa na uadilifu matabaka yote ya jamii ya nchi hiyo, badala ya kutumia mabavu.