JMEC yalaani machafuko ya ndani Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i17389-jmec_yalaani_machafuko_ya_ndani_sudan_kusini
Kamisheni ya kusimamia na kufuatilia makubaliano ya amani nchini Sudan Kusini, JMEC imekosoa vikali machafuko na ukandamizaji wa haki za binaadamu unaoendela kufanyika katika nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 14, 2016 04:34 UTC
  • JMEC yalaani machafuko ya ndani Sudan Kusini

Kamisheni ya kusimamia na kufuatilia makubaliano ya amani nchini Sudan Kusini, JMEC imekosoa vikali machafuko na ukandamizaji wa haki za binaadamu unaoendela kufanyika katika nchi hiyo.

Kamisheni hiyo kwa kifupi JMEC imetoa ripoti kuhusu machafuko na vitendo vya utumiaji mabavu vinavyoendelea kushuhudiwa nchini humo na kusema kuwa hali hiyo ni ukiukwaji wa wazi wa makubaliano ya amani. Imesisitiza kuwa, hali hiyo haiwezi kuvumilika. Mkuu wa kamisheni hiyo ambaye pia ni rais wa zamani wa Botswana, Festus Mogae, ametaka kufanyike kikao cha dharura tarehe 19 ya mwezi huu kwa lengo la kuchunguza hali ya mambo nchini Sudan Kusini.

Mahasimu wawili wanaopambana Sudan Kusini

Aidha amezitaka pande husika katika mapigano nchini humo kuanza upya mazungumzo kwa maslahi ya taifa lao. Amesisitiza kuwa, ni suala la kusikitisha mno kuendelea machafuko ndani ya taifa hilo changa zaidi barani Afrika.

Itakumbukwa kuwa Sudan Kusini ilitumbukia katika machafuko tangu mwaka 2013 baada ya Rais Salva Kiir wa nchi hiyo kumtuhumu makamu wake wa zamani Riek Machar kwamba alipanga mapinduzi dhidi yake. Mwezi Agosti mwaka jana pande mbili zilitiliana saini makubaliano ya amani ambayo hata hivyo mwezi Julai mwaka huu yalikiukwa baada ya kutokea mapigano makali mjini Juba, mji mkuu wa nchi hiyo.