Riek Machar: Nitarejea Sudan Kusini liwe liwalo
Kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini, Riek Machar amesema karibuni hivi atarejea nchini mwake akisitiza kuwa angali Makamu wa Rais wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.
Dakta Machar amesema wafuasi wake wa kundi la waasi wako tarayi kufanya mazungumzo na upande wa Rais Salva Kiir wa nchi hiyo ili kuupatia ufumbuzi mgogoro uliopo.
Machar ambaye kwa sasa yuko mjini Johannesburg nchini Afrika Kusini kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake amesema hana wasi wasi kuwa atarejea nchini mwake hivi karibuni na kwamba Rais Salva Kiir ndiye aliyeanzisha mapigano mapya mjini Juba mwezi Julai mwaka huu, kwa kuwa anaogopa kufanyika uchaguzi huru, ulio wazi na wa kidemokrasia.
Haya yanajiri siku chache baada ya Rais wa Sudan Kusini kutoa onyo kali dhidi Machar na kumtaka ajiweke kando na siasa pamoja na madaraka ya nchi hiyo. Alisema Machar anapaswa kuheshimu mwenendo na anga ya kisiasa inayotawala Sudan Kusini na aunge mkono serikali ya mpito na mchakato wa makubaliano ya amani.
Aidha Salva Kiir alibainisha kuwa, Machar ana haki ya kurejea nchini akiwa kama raia wa kawaida na si vinginevyo.
Hii ni katika hali ambayo, makumi ya wanajeshi wanaomuunga mkono Machar na wengine wanne waitifaki wa Rais Kiir waliuawa mwishoni mwa wiki katika mapigano yaliyojiri eneo la Malakal. Brigedia Lul Ruai Koang, msemaji wa SPLA amethibitisha habari hizo na kusema kuwa wapiganaji 56 wa kundi hilo la waasi waliuawa katika makabiliano hayo.