Raia Sudan Kusini waendelea kuuawa ovyo
Maafisa wa serikali ya Sudan Kusini wametangaza kuwa, raia wasiopungua 15 wameuawa katika kijiji kimoja kilichoko karibu na mji mkuu wa nchi hiyo, Juba.
Polisi ya serikali ya Sudan Kusini imetangaza kuwa, raia hao wameuawa katika machafuko yaliyotokea kwenye kijiji cha Mangalla kilichoko kaskazini mwa mji wa Juba.
Afisa wa polisi ya Sudan Kusini, Daniel Justine Bolo amesema kuwa, maiti za raia 15 wakiwemo wanawake wawili zimepatikana katika kijiji hicho na kwamba baadhi ya waliouawa ni raia wa nchi jirani ya Sudan.
Mauaji ya hapa na pale yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara nchini Sudan Kusini hususan katika mji mkuu wa nchi hiyo, Juba na maeneo ya kandokando yake.
Kutokana na hali hiyo nchi jirani zimetoa wito wa kutumwa kikosi cha kulinda amani huko Sudan Kusini na kuzuia mauaji na machafuko zaidi. Vilevile Umoja wa Mataifa umeitaka serikali ya Juba ikubali uamuzi wa kimataifa wa kutumwa askari 4,000 wa kieneo nchini humo kwa ajili ya kulinda amani na maisha ya raia.