AU yafanya uchunguzi kuhusu vitendo vya wanajeshi wake Somalia
-
Askari wa AMISOM nchini Somalia
Umoja wa Afrika AU umesema, umeanzisha uchunguzi wa kubaini ni katika mazingira gani, askari wa kikosi cha AMISOM nchini Somalia walifanya mauaji dhidi ya raia.
Francisco Madeira, mkuu wa kikosi cha AMISOM alitangaza habari hiyo jana na kuongeza kuwa, uchunguzi umeanza kuhusiana na kushambuliwa raia na wanajeshi wa Umoja wa Afrika huko Somalia. Ufyatuaji risasi huo ulifanyika wakati askari hao walipokuwa wanawapekua msafara mmoja wa watu ili kujua utambulisho wao.
Askari wa AMISOM wametumwa nchini Somalia kwa ajili ya kulinda raia, lakini mara kwa mara wamekuwa wakituhumiwa kuwashambulia raia. Miongoni mwa kesi hizo ni kuuawa raia wanne mwezi Aprili mwaka huu na kuuawa raia 14 mwezi Julai mwaka huu pia.
Karibu askari jeshi 22 elfu wa Umoja wa Afrika walitumwa nchini Somalia mwaka 2007 ili kupambana na kundi la kigaidi la ash Shabab.
Karibu miaka 25 sasa Somalia haina serikali kuu tangu alipopinduliwa dikteta Muhammed Siad Barre mwaka 1991. Tangu wakati huo machafuko yameikumba nchi hiyo ya Pembe ya Afrika na machafuko hayo yameziathiri pia nchi jirani ikiwemo Kenya.