Gordhan akataa kuzungumzia uungaji mkono wa ANC kwake
Waziri wa Fedha wa Afrika Kusini Pravin Gordhan leo amekataa kueleza iwapo ana imani na uungaji mkono wa kisiasa wa chama tawala cha ANC kwake, ikiwa imesalia chini ya wiki moja kabla ya kutakiwa kujibu mahakamani tuhuma zinazomkabili.
Waziri wa Fedha wa Afrika Kusini anatuhumiwa kuidhinisha kiufisadi kustaafu mapema kwa aliyekuwa Naibu Kamishna wa Kodi na kisha kumkodi tena afisa huyo kama mshauri na hivyo kuisababishia Mamlaka ya Kodi ya Afrika kusini gharama ya dola 79,000. Pravin Gordhan amekanusha tuhuma hizo na kusema kesi dhidi yake inachochewa kisiasa. Waziri wa Fedha wa Afrika Kusini jana aliulizwa swali bungeni iwapo bado ana matarajio ya kuungwa mkono kisiasa na chama tawala ANC wakati huu ambapo anakabiliwa na tuhuma za ufisadi au la naye akajibu kwa kusema kuwa hawezi kujibu swali hilo.