Serikali ya Nigeria yatakiwa kuongeza juhudi za kuwapokonya silaha wanamgambo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i18418-serikali_ya_nigeria_yatakiwa_kuongeza_juhudi_za_kuwapokonya_silaha_wanamgambo
Asasi isiyo ya kiserikali ijulikanayo kwa jina la Mercy Corps imeitaka serikali ya Nigeria kuunganisha nguvu zake na kuzitumia kwa ajili ya kuwapokonya silaha wanamgambo na kufanya juhudi za kuandaa mazingira mazuri ya kuwafanya wanamgambo hao wanaopokonywa silaha wakubalike katik ajamii.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 30, 2016 03:54 UTC
  • Serikali ya Nigeria yatakiwa kuongeza juhudi za kuwapokonya silaha wanamgambo

Asasi isiyo ya kiserikali ijulikanayo kwa jina la Mercy Corps imeitaka serikali ya Nigeria kuunganisha nguvu zake na kuzitumia kwa ajili ya kuwapokonya silaha wanamgambo na kufanya juhudi za kuandaa mazingira mazuri ya kuwafanya wanamgambo hao wanaopokonywa silaha wakubalike katik ajamii.

Taasisi hiyo isiyo ya kiserikali ilitoa mwito huo ljana Jumamosi mjini Abuja na kuongeza kuwa, mashambulizi ya wanamgambo wa Boko Haram yangali yanaendelea katika maeneo ya kaskazini na kaskazini mashariki mwa Nigeria, hivyo serikali ya nchi hiyo inapaswa, sambamba na kukabiliana na mashambulizi hayo, ifikirie pia hali ya baada ya kuwapokonya silaha wanamgambo wa genge hilo. Tamko la taasisi hiyo limesema, serikali ya Nigeria inapaswa kuliweka kwenye ajenda yake kuu suala la kuwapokonya silaha wanamgambo wa Boko Haram na kuwarejesha katika maisha ya uraiani.

Ghilda Chrabieh ni mmoja wa viongozi wa taasisi hiyo. Amesema, vijana wengi wa Nigeria hawana mbele wala nyuma, hivyo wanashawishika kiurahisi kujiunga na magenge ya kigaidi kama la Boko Haram, hivyo serikali ina wajibu wa kuwasaidia kifedha, kiroho na kisaikolojia vijana hao ili wasikubali kiurahisi kulaghaiwa na magenge ya wahalifu.

 

Aidha amesema, hadi hivi sasa serikali ya Nigeria imejaribu mara kadhaa kuendesha zoezi la kuwapokonya silaha wanamgambo na kuwarejesha katika maisha ya uraiani, lakini suala la kurejea uraiani wanamgambo hao waliopata mafunzo ya kijeshi ni changamoto nyingine kubwa kwa usalama wa maeneo wanakorejea.

Kundi la kigaidi la Boko Haram limekuwa likifanya mashambulizi tangu mwaka 2009 nchini Nigeria. Taasisi ya Mercy Corps inajishughulisha na migogoro ya kimaumbile, matatizo ya kiuchumi na mizozo ya ndani.