Kuongezeka vitendo vya utumiaji mabavu na ukatili nchini Sudan Kusini
Katika hali ambayo asasi za kimataifa zinafanya juhudi za kuhitimisha vitendo vya ukatili nchini Sudan Kusini, bado wimbi la vitendo hivyo vingali vinaendelea nchini humo.
Jumamosi ya juzi mwakilishi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika alifika maeneo yanayoshuhudia mapigano mjini Juba, mji mkuu wa nchi hiyo na kubaini sababu ya kuendelea mapigano ambapo alisisitizia umuhimu wa kutatuliwa migogoro ya usalama nchini humo. Machafuko ya kisiasa katika maeneo tofauti ya Sudan Kusini yanaendelea kushuhudiwa katika hali ambayo wanaomuunga mkono Riek Machar, kiongozi wa wapinzani nchini humo sanjari na kuanzisha eneo maalumu la kijeshi, wanajiimarisha kijeshi kwa ajili ya kukabiliana na mashambulizi tarajiwa dhidi yao.
Kuwasili mjumbe wa Umoja wa Afrika mjini Juba, kunajiri katika hali ambayo Jumamosi iliyopita, watu wenye silaha na wanaomuunga mkono Machar walishambulia shule mbili ambapo kwa akali wanafunzi 30 katika jimbo la Amadi kusini magharibi mwa nchi hiyo walitekwa nyara na kupelekwa kusikojulikana. Juhudi za askari wa usalama kwa ajili ya kuwatambua waasi waliohusika na utekaji nyara huo na pia hatma ya wanafunzi hao, bado zinaendelea. Hii ni katika hali ambayo wiki iliyopita Mahimbo Mdoe, mjumbe wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kushughulikia Watoto (UNICEF) nchini Sudan Kusini alitangaza kuwa, jumla ya watoto 145 wameachiliwa huru hivi karibuni kutoka makundi mawili moja likiwa ni la Riek Machar, makamu wa zamani wa Rais Salva Kiir na kundi la Cobra, huko katika mji wa Pibor mashariki mwa nchi hiyo. Kuongezeka machafuko nchini Sudan Kusini kunajiri katika hali ambayo siku chache zilizopita Rais Kiir alitoa onyo kwa hasimu wake Riek Machar kwamba sanjari na kulaani vitendo hivyo nchini, anatakiwa pia aendelee kuwa mbali na ulingo wa kisiasa.
Rais Salva Kiir anasisitiza kuwa, Machar hana haki ya kurejea nchini ispokuwa kwa anwani ya raia wa kawaida na si vinginevyo na kwamba lazima aheshimu sheria ya nchi. Katika radiamali yake, kiongozi huyo wa waasi na makamu wa zamani wa rais, amewataka wafuasi wake kuingia katika vita vikali dhidi ya serikali ya Rais Salva Kiir. Machafuko yanayoshuhudiwa katika maeneo tofauti ya Sudan Kusini, yamepelekea maelfu ya raia hususan watoto kukumbwa na hali mbaya ya kibinaadamu inayotia wasi wasi na kuzifanya asasi tofauti kutoa indhari juu ya kuendelea hali hiyo. Mashambulizi ya wabeba silaha wanaomuunga mkono Machar ambayo yamejiri siku za hivi karibuni katika barabara za mawasiliano na kistratijia za mji wa Yei, kusini magharibi mwa Sudan Kusini, yamesababisha zaidi ya watu 55 kuuawa na kujeruhiwa.
Shambulizi la hivi karibuni kabisa la wanamgambo hao ni hujuma dhidi ya magari manne yaliyokuwa yamewabeba raia katika eneo hilo ambapo watu 25 waliuawa. Kwa mujibu wa ripoti rasmi, makabiliano ya risasi na mashambulizi ya wabeba silaha baina ya Harakati ya Uhuru kwa ajili ya Watu wa Sudan Kusini wanaoongozwa na Riek Machar na askari wa serikali yaliyojiri nje ya ikulu ya rais, yameirejesha nchi hiyo katika wimbi la machafuko hofu na wasi wasi mkubwa. Zeid bin Ra'ad, Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa amenukuliwa akisema kuwa, kuendelea mwenendo wa hivi sasa nchini humo na kadhalika kuenea vitendo vya ukatili na visivyokuwa na huruma dhidi ya watu wa kaumu tofauti, ni jambo hatari sana ambalo athari zake haziwezi kufidiwa. Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amewataka viongozi wa kisiasa na kikabila nchini Sudan Kusini, kujizuia na kujiepusha na vitendo vinavyozidisha mivutano nchini humo.