Machafuko ya umwagaji damu yaendelea kushuhudiwa Burundi
Machafuko na mapigano ya umwagaji damu yameendelea kushuhudiwa nchini Burundi.
Msemaji wa Polisi ya Burundi Pierre Nkurikiye amevieleza vyombo vya habari kuwa watu sita walioshukiwa kuhusika na wizi walishambuliwa na kujeruhiwa vibaya na wakaazi wa eneo la Matongo mkoani Kayanza kaskazini mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa Nkurikiye washukiwa hao walifikishwa kituo cha polisi cha karibu. Hata hivyo mmoja wa watu hao amefariki dunia kutokana na majeraha makubwa aliyopata.
Hii ni katika hali ambayo wapinzani wa serikali ya Bujumbura wanasema mapigano na machafuko hayo yametokana na sababu za kisiasa.
Imeelezwa kuwa wanachama wa tawi la vijana la chama tawala wamewatuhumu kuhusika na wizi watu hao ambao ni wafuasi wa upinzani bila ya kuwa na ushahidi wowote.
Ghasia, machafuko na umwagaji damu ulianza kushuhudiwa nchini Burundi mwezi Aprili mwaka jana na kushtadi baada ya Rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza kuamua kugombea urais kwa muhula wa tatu, hatua ambayo wapinzani wanasema ni kinyume na katiba na makubaliano ya amani yaliyofikiwa Arusha, Tanzania.
Mamia ya watu wameuawa na maelfu ya wengine wamelazimika kuyahama makazi yao na kutafuta hifadhi katika nchi jirani ili kunusuru maisha yao.../