Sudan yakosoa kurefushwa vikwazo dhidi yake na Marekani
Serikali ya Sudan imekosoa vikali hatua ya Marekani ya kuirefushia vikwazo Khartoum kwa muda wa mwaka mmoja mwingine.
Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Sudan iliyotolewa leo Jumanne imesema kuwa, vikwazo hivyo sio vya kiadilifu na kwamba sababu zinazotolewa na Marekani za kuongeza muda wa vikwazo hivyo dhidi ya Khartoum ni za kusikitisha. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, vikwazo hivyo ni vya upande mmoja ambavyo misingi yake ni madai ya urongo na yasiyokuwa na mantiki.
Rais Barack Obama wa Marekani hapo jana aliongeza muda wa vikwazo kwa nchi hiyo ya Kiafrika kwa mwaka mmoja zaidi, akisema kuwa sera za utawala wa Khartoum zinaendelea kuwa tishio kwa usalama wa Marekani sanjari na kukinzana na sera za Washington.
Hata hivyo taarifa ya ubalozi wa Marekani mjini Khartoum imesema kuwa uamuzi wa Washington kurefusha vikwazo hivyo ni wa kiufundi na kwamba yumkini vikalegezwa.
Tangu mwaka 1997 hadi sasa serikali ya Marekani imeiwekea Sudan vikwazo vya kiuchumi, ambavyo vimekuwa vikiongezwa muda wake kila mwaka.
Marekani ambayo imekuwa mstari wa mbele kuziwekea vikwazo nchi nyingine kwa visingizio mbalimbali kama ukiukwaji wa haki za binadamu na kadhalika, yenyewe ni muungaji mkono mkubwa wa utawala wa Kizayuni wa Israel ambao unatenda jinai kubwa na za kila leo huko Palestina.