Umoja wa Mataifa wakiri vikosi vyake kushindwa kuwalinda raia Sudani Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i18658-umoja_wa_mataifa_wakiri_vikosi_vyake_kushindwa_kuwalinda_raia_sudani_kusini
Umoja wa Mataifa umetangaza na kukiri kwamba, vikosi vyake vya kulinda amani huko Sudani Kusini vilishindwa kuwalinda raia katika mji mkuu Juba wakati wa mapigano baina ya pande mbili mwezi Julai mwaka huu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 02, 2016 04:32 UTC
  • Umoja wa Mataifa wakiri vikosi vyake kushindwa kuwalinda raia Sudani Kusini

Umoja wa Mataifa umetangaza na kukiri kwamba, vikosi vyake vya kulinda amani huko Sudani Kusini vilishindwa kuwalinda raia katika mji mkuu Juba wakati wa mapigano baina ya pande mbili mwezi Julai mwaka huu.

Uchunguzi uliofanywa na Umoja wa Mataifa unaonyesha kuwa, vikosi vyake vya kusimamia amani huko Sudan Kusini vilikuwa na utendaji dhaifu katika kukabiliana na machafuko yaliyoibuka mwezi Julai mwaka huu mjini Juba na kwamba, askari hao wa kulinda amani walishindwa kuwalinda raia mkabala na mashambulio.

Aidha uchunguzi huo wa Umoja wa Mataifa unaeleza kuwa, askari hao wa UN hawakuonyesha radiamali inayotakiwa katika shambulio la tarehe 11 Julai la wanajeshi wa Sudan Kusini dhidi ya hoteli walimokuwemo wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa.

Ban Ki-moon Katibu Mkuu wa UN na Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini

Tayari Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki- Moon amemfuta kazi kamanda wa kikosi hicho baada ya utafiti wa ndani kubaini kuwa vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa huko Sudan Kusini vilikataa kujibu mashambulizi, wakati wanajeshi wa serikali walipowashambulia wafanyakazi wa mashirika ya kigeni ya misaada.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alitangaza jana kwamba, amemfuta kazi Meja Jenerali Johnson Mogoa Kimani Ondieki raia wa Kenya baada ya kikosi alichokuwa akikiuongoza huko Sudan Kusini kushindwa kuwalinda raia dhidi ya mashambulio.