Upinzani: Matokeo ya kura ya maoni Kodivaa ni bandia
Wapinzani nchini Ivory Coast wamepuuzilia mbali matokeo ya kura ya maoni ya kupitisha au kukataa katiba mpya ya nchi na kusema kuwa matokeo hayo ni bandia na ambayo hayaakisi sauti ya wananchi walio wengi.
Hii ni baada ya Tume ya Uchaguzi nchini humo kutangaza matokeo rasmi ya zoezi hilo lililofanyika Oktoba 30 yaliyobainisha kuwa, asilimia 93 ya mamilioni ya wananchi waliopiga kura hiyo ya maoni wanaiunga mkono katiba hiyo. Kwa mujibu wa tume hiyo, asilimia 42 ya watu milioni 6.3 waliotimiza masharti ya kupiga kura wameshiriki zoezi hilo la kidemokrasia, huku upinzani ukidai kuwa ni asilimia 10 tu ya wapiga kura ndio walioshiriki.
Pascal Affi Nguessan, mkuu wa chama cha upinzani cha Ivorian Popular Front (FPI) amesema matokeo hayo ya kura ya maoni hayaendani na idadi ndogo ya wapiga kura waliojitokeza kushiriki zoezi hilo.
Hata hivyo Joel N'Guessan, msemaji wa chama tawala cha Rally of Republicans Party (RDR), ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, zaidi ya asilimia 90 ya wananchi walioshiriki kura hiyo wameiunga mkono katiba hiyo mpya na kwamba hilo linadhihirisha wazi kuwa wananchi wa Kodivaa wanataka kufungua ukurasa mpya wa uongozi, siasa na uendeshaji wa mambo nchini humo.
Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast anasema katiba hiyo mpya itadhamini amani katika nchi hiyo iliyoathiriwa na machafuko ya kisiasa kwa miaka kadhaa.
Wapinzani nchini Ivory Coast walisusia kushiriki katika kura hiyo ya maoni ya kuainisha katiba mpya wakisema kuwa, rasimu hiyo ya katiba imebuniwa ili kuuimarisha zaidi muungano wa kisiasa wa Rais Alassane Ouattara. Katiba ya hivi sasa ya Kodivaa ambayo iliandaliwa chini ya utawala wa kijeshi baada ya mapinduzi ya mwaka 1999, imekuwa ni sababu kuu ya machafuko ya muda mrefu katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.