Nov 04, 2016 15:50 UTC
  • Mashia Nigeria: Hujuma dhidi yetu ni mwangwi wa Uwahabi nchini

Waislamu wa madhehebu ya Shia huko Nigeria wamekosoa vikali ukandamizaji unaofanywa dhidi yao na vyombo vya usalama nchini humo na kusisitiza kuwa, dhulma hizo zimetokana na fikra za Kiwahabi.

Abdul Giwa, msemaji wa Harakati ya Kiislamu Nigeria amesema vyombo vya dola vimeanzisha 'kampeni ya umwagaji damu na uharibifu' dhidi ya Mashia wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika, na kwamba harakati hizo zimechochewa na idiolojia ya Uwahabi ambayo chimbuko lake ni Saudi Arabia.

Giwa ameliambia shirika la habari la Reuters kama tunavyomnukuu: "Tuna uhuru na haki ya kuabudu, kinachotakiwa kufanywa na serikali ni kutudhaminia usalama, kutuelewa na kutotuhujumu."

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria (Kushoto) na Mfalme wa Saudi Arabia, Salman bin Abdulaziz Aal Saud

Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Oktoba 23, mkutano wa kuzuia harakati za Mashia nchini Nigeria ulifanyika katika jimbo la Kano, na kuwaleta pamoja mamufti wa Kiwahabi pamoja na mkuu wa harakati ya 'Izaalatul- Bida'a wa Ihyaaus-Sunna' mwenye mahusiano ya karibu na utawala wa kifalme wa Saudia. Siku chache kabla ya hapo, Mawahabi wenye mafungamano na utawala wa Aal-Saud sanjari na kushambulia nyumba ya Sheikh Adamu Tsoho Ahmad, mjumbe wa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini humo, waliichoma moto pia Husseiniyya ya Mashia mbali na kuua makumi ya Waislamu wa madhehebu hiyo.

Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu Nigeria baada ya kushambuliwa na wanajeshi Disemba mwaka jana

Kamisheni ya Haki za Binadamu za Kiislamu (IHRC) yenye makao yake mjini London Uingereza hivi karibuni ilitangaza kuwa, nyaraka zilizofichuliwa na mtandao wa WikiLeaks zinathibitisha kwamba utawala wa Riyadh unashiriki moja kwa moja katika kukandamiza Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria.

Tags