Polisi Kongo DR wazima maandamano ya wapinzani Kinshasa
Maafisa wa polisi wa kupambana na ghasia wametumia mabomu ya kutoa machozi kuzima maandamano ya wapinzani katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kinshasa.
Maafisa hao wa usalama waliizingira nyumba ya kiongozi wa upinzani nchini humo Mzee Etienne Tshisekedi katika wilaya ya Limete, viungani mwa mji mkuu Kinshasa hapo jana, ambapo makundi ya wafuasi wa upinzani yalikuwa yamekusanyika tayari kwa maandamano dhidi ya serikali ya Rais Joseph Kabila.
Kadhalika vyombo vya usalama vilikata mawasiliano sambamba na kuzima mawimbi ya Idhaa ya Radio ya Kimataifa ya Ufaransa pamoja na Radio Okapi, inayofadhiliwa na Umoja wa Mataifa.
Polisi ya Kongo imepiga marufuku maandamano ya aina yoyote ya kisiasa kufuatia kuongezeka mivutano ya kisiasa nchini humo katika siku za hivi karibuni katika miji mbalimbali ya nchi, kufuatia uamuzi wa Rais Joseph Kabila wa kutaka kubakia madarakani baada ya kumalizika kipindi cha uongozi wake.
Wapinzani nchini Kongo wanamtaka Rais Kabila aondoke madarakani muda wake wa kuwepo uongozini utakapomalizika mwishoni mwa mwaka huu na kusisitiza kuwa lazima uchaguzi wa rais ufanyike mwakani. Hata hivyo kulingana na uamuzi uliotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya makubaliano yaliyofikiwa katika mazungumzo ya kitaifa hivi karibuni kati ya chama tawala na vyama vidogo kadhaa vya upinzani, uchaguzi wa rais umepangwa kufanyika mwaka 2018.