Malema ataka sheria ya ardhi ya kipindi cha Apartheid ifutwe
Kiongozi wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) ambaye anataka kutaifishwa mabenki, migodi na ardhi nchini Afrika Kusini amesema kuwa, atashinikiza Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo itupilie mbali sheria ya ardhi ya kipindi cha utawala wa ubaguzi wa rangi (apartheid) inayotumiwa dhidi yake mahakamani kutokana na kutoa wito wa kutwaliwa mashamba makubwa ya kilimo yanayomilikiwa na wazungu waliowachache.
Julius Malema anataka sheria ya 1956 Riotous Assemblies itupiliwe mbali, suala ambalo wataalamu wanasema kuna uwezekano mkubwa likafanikiwa.
Malema alifikishwa mahakamani jana Jumatatu katika mji wa Newcastle kwenye jimbo la KwaZulu-Natal akikabiliwa na mashtaka ya kuchochea wafuasi wake kuvamia na kutwaa mashamba yanayomilikiwa na wazungu tangu zama za kipindi cha ubaguzi wa rangi, jambo ambalo ni kinyume na sheria ya ardhi ya 1956 Riotous Assemblies.
Marekebisho ya ardhi ni miongoni mwa masuala nyeti sana nchini Afrika Kusini na yalizusha mjadala mkubwa baada ya kupungua mazao ya kilimo katika nchi jirani ya Zimbabwe kufuatua hatua ya serikali ya Rais Robert Mugabe ya kuwafukuza wakulima wazungu kwenye mashamba ya kilimo cha biashara.
Chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) kinachoongozwa na Julius Malema kina viti 25 kati ya viti vyote 400 vya Bunge la Afrika Kusini.