Kenya yaanza kuondoa askari wake wa kulinda amani Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i19177-kenya_yaanza_kuondoa_askari_wake_wa_kulinda_amani_sudan_kusini
Kundi la kwanza la askari wa Kenya waliokuwa wakihudumu katika operesheni ya Umoja wa Mataifa ya kulinda amani nchini Sudan Kusini (UNMISS) walirejea nchini mwao hapo jana baada ya serikali ya Nairobi kuwaamuru waondoke nchini humo kufuatia kutimuliwa kamanda wa Kenya aliyekuwa akiongoza operesheni hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 10, 2016 00:08 UTC
  • Kenya yaanza kuondoa askari wake wa kulinda amani Sudan Kusini

Kundi la kwanza la askari wa Kenya waliokuwa wakihudumu katika operesheni ya Umoja wa Mataifa ya kulinda amani nchini Sudan Kusini (UNMISS) walirejea nchini mwao hapo jana baada ya serikali ya Nairobi kuwaamuru waondoke nchini humo kufuatia kutimuliwa kamanda wa Kenya aliyekuwa akiongoza operesheni hiyo.

Kwa amri ya Rais Uhuru Kenyatta, Kenya ilitangaza wiki iliyopita kuwa itawaondoa askari wake hao baada ya ripoti ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuituhumu UNMISS kwamba ilizembea kwa kushindwa kukabiliana na shambulio la mwezi Julai dhidi ya hoteli moja katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba. Tuhuma hizo zilisababisha kutimuliwa kamanda wa UNMISS kutoka Kenya Luteni Jenerali Johnson Mogoa Kimani Ondieki.

Luteni Jenerali Johnson Mogoa Kimani Ondieki

Msemaji wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS Shantal Persaud amethibitisha kuwa serikali ya Kenya imeanza zoezi la kuwaondoa askari wake katika mji wa Wau ulioko kaskazini magharibi mwa Sudan Kusini.

"Leo tumeanza kujiondoa Sudan Kusini" alisema Meja Jenerali Benjamin Biwott hapo jana mbele ya waandishi wa habari katika uwanja wa ndege wa kimataifa mjini Nairobi baada ya askari wapatao 100 kuwasili nchini.

Aliongeza kuwa makundi ya askari wengine wa kikosi cha askari wapatao 1,000 wa nchi hiyo waliokuwa huko Sudan Kusini watawasili nchini mnamo siku zijazo, ingawa hakubainisha muda halisi wa kukamilika zoezi la kuwaondoa askari hao kutoka kwenye kikosi cha UNMISS chenye jumla ya askari wapatao 12,000.

Kwa mujibu wa Meja Jenerali Biwott, askari wa Kenya wamehudumu katika operesheni za kulinda amani katika nchi 44 katika kipindi cha miongo minne iliyopita na kwamba nchi hiyo itaendelea kutekeleza jukumu lake hilo katika nchi nyinginezo.

Shambulio la mwezi Julai dhidi ya hoteli mjini Juba lilitokea baada ya siku kadhaa za mapigano baina ya vikosi vitiifu kwa Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na vile vya aliyekuwa Makamu wake na hasimu wake mkuu wa kisiasa Riek Machar.../